Mbinu Kumi(10) Za Kuepuka Kuchoka Sana 2015.

Bado tupo kwenye mwanzo wa mwaka, na mwanzo wa mwaka kila mtu anakuwa na nguvu kubwa sana ya kufanya majukumu yake. Huu ni muda ambao kila mtu anakazana kujaribu kutimiza malengo yake.

Kadiri siku zinavyozidi kwenda watu wengi huanza kuchoka na mpaka kuja kufika mwezi wa kumi au kumi na moja asilimia kubwa ya watu wanakuwa wamechoka sana kiasi cha kushindwa kuwa na uzalishaji mzuri.

Hali hii ina madhara sana katika ufanisi wetu wa kazi na hata biashara. Na kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuwa kwenye ufanisi mkubwa kwa angalau mwaka mzima au wiki 50 kati ya wiki 52 za mwaka.

Leo hapa UTAJIONGEZA na mbinu 10 za kuepuka kuchoka sana mwaka huu 2015.

1. Upe mwili wako kazi. Kama kazi zako ni za ofisini au za kukaa, kufanya hivyo kila siku kutaufanya mwili wako uwe hovyo sana. Hivyo ni vyema kuupa mwili wako kazi, fanya mazoezi, cheza, tembea, kimbia, na hii ni kila siku.

2.Pata muda wa kutosha wa kulala. Kulingana na kazi zako unaweza ukasema huwezi kupata muda wa kutosha wa kulala, ila kulala kutaufanya mwili wako kuwa na nguvu na hata akili yako kuwa na ubunifu. Anza kulala nusu saa kabla ya muda wako wa kawaida wa kulala. Pia pata muda kidogo wa kulala mchana kama inawezekana kwako.

3. Pata dakika tano za kufanya tajuhudi/taamuli.

Hizi ni dakika chache ambapo unakaa kimya na kuondoa mawazo yote kwenye kichwa chako. Njia rahisi ya kufanya hili ni kukaa sehemu iliyotulia na kufunga macho yako kisha kuanza kuhesabu pumzi zako. Itakusaidia sana kusafisha akili yako.

4. Weka orodha ya vitu unavyoshukuru kuwa navyo. Haijalishi una matatizo kiasi gani kuna vitu unafurahi kuwa navyo, huenda ni familia inayokupenda, huenda ni biashara nzuri. Weka orodha hii na ipitie kila siku.

5. Kuwa na muda maalumu usiku ambapo unazima vifaa vyako vyote, yaani kompyuta, simu, tv na chochote kile. Fanya muda wako wa kupumzika kuwa wa kupumzika kweli.

6. Kuwa na picha inayokupa furaha na kukuhamasisha. Inaweza kuwa picha ya mtoto wako au kitu chochote. Itumie picha hii pale unapoona uvivu wa kufanya jambo.

7. Jisamehe. Kuna makosa mengi umeyafanya kwenye maisha yako, acha kuendelea kujitesa, jisamehe na songa mbele.

8. Kuwa mkarimu, wasaidie wengine, utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

9. Tumia kipaji ulichonacho. Hata kama kazi au biashara unayofanya sio inayohusisha kipaji chako, tenga muda ambao utafanya kipaji chako. Kwa kufanya hivi utakuwa na nguvu na hamasa kubwa utaporudi kwenye kazi yako.

10. Fanya jambo moja kwa wakati. Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kutachangia wewe kuchoka haraka sana. Fanya jambo moja likiisha ndio uanze jambo jingine.

Hizi ni mbinu rahisi unazoweza kuanza kuzitumia leo ili kuhakikisha mwaka mzima unakuwa na ufanisi mkubwa sana.

Nakutakia kila la kheri.

0 comments: