Hatua Nne Muhimu Unazohitaji Kupitia Ili kufikia Mafanikio Makubwa 2015.

Mwaka umeanza na mwaka unakaribia kukomaa. Kila mwanzo wa mwaka watu wengi huweka malengo mablimbali ya kufanya kwenye mwaka husika. Huenda na wewe umeweka malengo mengi kama ambavyo umekuwa ukifanya miaka iliyopita.

Lakini pia watu wengi wanaoweka malengo huwa hawayafanyii kazi hata kidogo. Zaidi ya asilimia 85 ya watu wanaoweka malengo husahau malengo yao wiki sita baada ya mwaka mpya.

Ili na wewe usiwe mmoja wa watu ambao wanasahau malengo yao au wanashindwa kuyafikia kuna hatua nne muhimu za kufuata ili kuhakikisha unafikia mafanikio makubwa kwenyemaisha yako.

Hatua hizo nne ni kama ifuatavyo.

1. Amua ni nini unataka kwenye maisha yako.

Ni lazima uamue ni kitu gani hasa unataka kwenye maisha yako. Jua kwa usahihi na kwa uhakika na uweze kusema kwa sentensi fupi ni nini unataka kwenye maisha yako.

2. Amua ni gharama gani upo tayari kulipa.

Kama ulikuwa hujui ni kwamba HAKUNA KITU CHA BURE, yaani huwezi kupata kitu pasi na kutoa kitu. Hivyo ili uweze kupata kile unachotaka kwenye maisha lazima uwe tayari kulipa gharama. Inaweza kuwa unahitaji kufanya kazi zaidi, au gharama nyingine yoyote.

3. Weka vipaumbele vyako.

Baada ya kuamua unataka nini, na baada ya kujua ni gharama gani upo tayari kulipa, weka vipaumbele vyako. Amua ni vitu gani utafanya na vingine vyote sema hapana. Jifunze kusema hapana itakusaidia sana kwenye maisha yako.

Soma; Mambo 30 ya kusema hapana mwaka 2015.

4. Fanya kazi.

Yote hayo tuliyojadili hapo juu yanachangia asilimia 1 ya mafaniko. Asilimia 99 ya mafanikio yako itatokana na kazi. Ni lazima ufanye kazi sana, hakuna longolongo hakuna janja janja.

Soma; Misingi mitatu ya kujijengea mwaka 2015.

Fuata hatua hizo nne na anza haraka kufanyia kazi malengo yako. Nina hakika utaweza kufikia mafanikio makubwa. Ila kumbuka kwamba itakuchukua muda, maana mafanikio sio kitu cha kutokea papo kwa hapo.

Nakutakia kila la kheri,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

 

0 comments: