Je Vijana Wanaoingia Kwenye Siasa Wanaweza Kuwa Wakombozi Wetu?

Kumekuwa na wimbi kubwa la vijana hapa Tanzania ambao wanaingia kwenye siasa. Na kwanzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo baadhi ya vijana waliogombea ubunge walipata kuchaguliwa kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa vijana kuingia kwenye siasa.

Na hata kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 vijana wengi wameonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali. Na kwa kuwa mpaka sasa hatuna sheria inayoruhusu mgombea binafsi, vijana hawa wote ambao wana nia ya kugombea inawalazimu kupitia vyama vya siasa. Kwa sasa tuna vijana wengi sana ambao wameingia kwenye vyama mbalimbali vya siasa na wengine wamepata nafasi kubwa kwenye vyama hivi.

siasa

Swali kubwa la kujiuliza ni je vijana wengi kuingia kwenye siasa wanaweza kuwa wakombozi wa nchi yetu Tanzania? Natumia neno ukombozi kwa sababu naamini nchi yetu inahitaji ukombozi ili kutoka hapa ilipo. Inahitaji ukombozi kwa sababu tumefika hapa tulipo kutokana na uongozi mbovu na siasa na sera mbovu zilizowekwa na viongozi hawa wabovu. Na ukiangalia viongozi hao umri wao umekwenda sasa na hivyo vijana ndio watakwenda kuchukua nafasi zao siku za mbeleni.

Najiuliza swali hili kwa sababu tumeona baadhi ya vijana ambao wameingia kwenye siasa hizi wakiishia kutumiwa na baadhi ya watu na hivyo kujikuta wakishindwa kuleta mabadiliko yoyote. Tumeona baadhi ya vijana ambao walikuwa wakilalamikia uongozi mbovu ila wamepewa uongozi kwenye sehemu mbalimbali na kushindwa kuleta mabadiliko yoyote. Na vibaya zaidi wanaishia kuwa sehemu ya kitu walichokuwa wanakipinga.

Sina tatizo na kijana ambaye ameingia kwenye chama chochote cha siasa alichopenda yeye. Iwe ameingia CCM, CHADEMA, CUF au hata CHAUSTA. Kikubwa ambacho wananchi wanataka kuona ni mabadiliko ya kweli katika siasa zetu na hatimaye uongozi wa nchi yetu. Naamini mabadiliko haya yanawezekana kupitia vijana kama watajua ni kitu gani wanakwenda kufanya kwenye siasa hizi na kuepuka kutumika na wale ambao wapo kwenye mifumo hii kwa muda mrefu.

Wewe kama ni kijana ambaye umeingia kwenye siasa jiulize swali hili mara kwa mara na hakikisha unakuwa sehemu ya mabadiliko popote unapokuwepo.

Nakutakia kila la kheri katika harakati za kuleta mabadiliko katika taifa letu Tanzania.

TUKO PAMOJA.

Hakikisha hukosi makala mpya kila inapowekwa kwenye blog hii. Weka email yako hapo juu ili upate makala moja kwa moja kwenye email yako.

0 comments: