Mambo Matatu Ya Kuzingatia Katika Msamaha.

Msamaha una pande mbili kuwasamehe waliokukosea na kusamehewa na wale uliowakosea. Ni tendo linalotokana na wawili ,mmoja amekosa na wa pili amekosewa. Hivyo Kusamehe au kusamehewa ndio msamaha ambao huweza kuleta maelewano kati ya pande hizo mbili yaani mkosaji na mkosewa .

Tatizo kubwa la mwanadammu ni ile tabia ya kutokukubali kosa. Watu wengi wanashindwa kusamehe au kukubali msamaha kwa sababu hawajui maana ya msamaha. Kusamehe sio kusema, bali ni zaidi ya kutamka kwa mdomo. Kusamehe ni kumaliza chuki yote na maumivu yote yaliyo ndani ya moyo. Pande hizi mbili zikisameheana ( mkosaji na mkosewa ) makosa yote hufutwa na haibakii tena hatia juu yao kutokana na makubaliano yaliyofanyika kati ya hao wawili.

YAJUE MAMBO MATATU AMBAYO LAZIMA YATOKEE KATIKA MSAMAHA WA KWELI

  1. KUMPENDA ALIYEKUKOSEA

Upendo huu sio ule wa mdomoni bali wa kutoka ndani na kutokuwa na uchungu tena moyoni, hasa kusaidiana katika shida na raha ili kudumisha upendo. Wapo watu wengi waliosema wanasamehe lakini hawana mawasiliano na wale waliowakosea, huu sio msamaha, kumpenda aliyekukosea itakufanya uwe huru.

  1. KUSAHAU KOSA

Ingawa kibinadamu inaonekana ni vigumu kusahau kosa ulilotendewa lakini mbele ya Mungu inawezekana . Hivyo basi ukijiona kuwa umetoa msamaha au umepokea msamaha lakini kosa lililotendeka bado linakurejea katika akili yako basi ujuwe msamaha huo bado haujawa msamaha. Jitaidi kusahau,rudisha moyo wa ukarimu juu yake ili kuboresha mawasiliano ya awali.

  1. KUMWOMBEA

Yampasa mtu aliyetoa msamaha wa kweli amwombee Yule aliyemkosea, sio kumlaani bali ni kumshauri na kumwombea baraka ili afanikiwe katika maisha yake. Watu wengine huwaombea adui zao mabaya huo sio msamaha unapomwombea mwenzako nawe unabarikiwa na kusahau kosa.

HASARA ZA KUTOSAMEHE

Kuna hasara nyingi sana kama mtu hujasamehe na hizi ni baadhi tu,

1. Tunajifungia milango ya baraka sisi wenyewe

2. Unashindwa kufikiria maendeleo

3. Unakuwa na chuki na maumivu moyoni mwako

4.Unakosa afya njema

5.unakuwa mtu wa mawazo tu

Hivyo basi kutosamehe katika maisha yetu tunajizibia milango ya baraka katika maisha yetu,mwandishi wa kitabu cha The Miracle of your Mind anasema kuwa ‘’ Do not poison yourself through hatred, begin to forgive’’ Maana ni kwamba usijiwekee sumu mwenyewe kwa kupitia chuki, pia ametuasa tuanze sasa kusamehe.

‘’The feeling of wealth produces wealth, the feeling of being successful produces success’’ hivyo basi hisia za kitajiri au mali huzaa mali au utajiri vivyo hivyo katika hisia za chuki huzaa chuki na siyo mafanikio, weka sana akilini mwako maneno hayo kila mara katika maisha yako.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali unaweza ukawasiliana naye kupitia simu 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com

0 comments: