Ulizaliwa Uishi Wewe, Usiishi Kwa Ajili Ya Wengine.

Kila mtu alivyoumbwa kuna kitu alizaliwa ili aje kukifanya, analo jibu la changamoto fulani katika maisha haya tulimo. Ni wajibu wa kila mmoja kuweza kutambua hilo na kuishi hilo kusudi. Hakuna hata mtu mmoja aliyezaliwa ili aje kuwa kama mtu mwingine, ulizaliwa uwe wewe. Kila mtu ni wa pekee ana uwezo wa kufanya mambo kwa namna yake ambayo hakuna mwingine anaweza kufanya hivyo.
Hata mimi uandishi wangu wa makala hauwezi kufanana na wa mwingine, ninayo namna yangu ya kuandika ambayo Mungu aliiweka na naenenda kwa hiyo. Nikijaribu kuwa kama mwingine au kuiga nitashindwa tu, inabidi niwe mimi. Ni wajibu wa kila mtu kwa imani yake kuweza kugundua kile ameumbiwa kufanya.
Kuna mwingine amezaliwa kufundisha wengine tu, popote alipo ualimu wake utaonekana tu, yaani atafurahia kufundisha tu hata kama hamna kipato anapata lakini yeye kuna amani anaipata ndani mwake, kuna kile kitu unaweza kufanya bila kutanguliza malipo, kile ambacho usipofanya unasikia kama una deni, unaona haujatimiza wajibu wako sawasawa. Ukishagundua kusudi la wewe kuwepo ni wajibu wako wewe mwenyewe kulisimamia na kuliishi hilo, ukimshirikisha Muumba wako katika kila hatua.
Pengine baada ya kugundua kusudi lako ni lipi, unaweza kukutana na vikwazo vingi katika kuliishi hilo kusudi. Ndugu yangu tambua kwamba ni wewe na Mungu wako mnaelewa hilo kusudi hivyo usitegemee kila mtu akuelewe kirahisi, usishangae kuona uliotegemea wakuelewe wasipokuelewa. Na hiyo isiwe sababu ya wewe kuona labda umepotea au hauko sawasawa, hata mimi kuweza kuandika hata makala yenye maneno hata mia mbili tu haikuwa rahisi mwanzoni. Kuna wakati nilipompa mtu ambaye nadhani ni wa karibu aipitie na kunipa maoni nilipata maoni ya kukatisha tamaa sana, lakini uzuri ni kwamba wapo waliolewa na kunitia moyo. Lakini si vyema kumpuuza anayekupinga pia maana walikuwa na sababu zao za msingi pia, mwingine anakuambia hujawahi kusomea uandishi au wewe na ufundi wako na uandishi wa makala kama hizi vinahusianaje? Waliona hivyo , hawakubahatika kuona kile kimewekwa ndani mwangu Lakini mimi ndio nilijua kwa nini naandika, maana naamini siandiki ili kupoteza muda wangu bali kuna mtu akisoma anapata uwezo wa kusogea hatua moja mbele, kuna badiliko linatokea ndani mwake, kuna maisha ya mtu yanaguswa na kumfanya awe mtu bora zaidi, na ndiyo furaha yangu hiyo.
Hivyo haijalishi unakutana na nini, naomba kama kweli una uhakika ndicho kitu umeitiwa endelea kufanya, ng’ang’ana tu wapo watakaokuelewa baadae, kuna watu mtoto akizaliwa wanashindwa kuelewa kama anafanana na nani lakini kadri anavyoendelea kukua wanamtambua vizuri na kuzidi kumfurahia hata kama mwanzoni hawakumkubali.
Kuna mtu anajua kabisa anachokifanya sicho kitu anatakiwa kufanya lakini anafanya tu kwa kuwa kuna watu wanamtaka afanye hilo. Wakati mwingine hata mzazi anaweza kukutaka uwe mtu fulani kwa sababu zake binafsi na pengine nzuri tu. Mwingine anaweza kukutaka ufanye kitu fulani kwa manufaa yake. Ishi wewe vile ulikusudiwa kuwa, tumia hekima na busara kuwaelewesha wanaotaka uwe tofauti na ulivyo wakati wewe una uhakika hivyo ndivyo unavyopasa kuwa. Wakati mwingine ikibidi ni bora unyamaze na kuwaacha waone kwa vitendo kile unamaanisha maana hauwezi kujieleza kwa kila mtu.
Hivyo ni wajibu wako na uamuzi wako wewe kwa kuwa ndiwe unajua nini unataka, kuamua kwa dhati kusimamia na kufanya kile unafurahia kufanya, kile kinakupa amani moyoni, kile unakifanya bila kuhangaika au kutumia nguvu nyingi zaidi. Kumbuka kuogopa kufanya kitu unachokipenda kwa kuhofia watu watasemaje haikupi wewe furaha wala amani, bali itakufanya wewe kuwa mtumwa wa nafsi yako mwenyewe, hauishi wanavyotaka watu au jamii, unatakiwa kuishi kama Mungu alivyokukusudia uwe, Ukijaribu kutimiza matakwa ya wanadamu unatakiwa ujue kuwa wanabadilika kila leo, leo wanaweza kukukubali na kukupenda kwa kuwa unafanya hilo lakini using’ang’ane leo watu hao hao wakikugeuka.
Hivyo tafuta sana kujijua wewe ni nani? Kwanini upo? Ukilijua kusudi lako basi liishi hilo kusudi lako , ni kwa kufanya hivyo utaweza kupata ile amani ya kweli maishani mwako, na pia kwa kuishi lile kusudi uliloumbiwa hautumii nguvu nyingi sana ili kuwa hapo, ukishajitambua mambo mengine yote yanakuwa yasharahisishwa, ukiwa kwenye mkondo wa maji, maji yakiwepo yatakupitia tu. Wajibu wako ni kutafuta mkondo wa maji ulipo.
Makala hii imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
Namba ya simu : +255 755 350 772

0 comments: