Sehemu Tano Unazoweza Kupata Mtaji Wa Kuanzia Biashara.

Kisingizio kikubwa cha watu kushindwa kuanza biashara kimekuwa ni mtaji. Kila siku watu wanalalamika wanapenda kuanza biashara ila mtaji hawana. Lakini wakati huo hawafanyi jitihada zozote za kupata mtaji huo au kuanza kidogo na kufikia makubwa.

Kulalamika kwamba taasisi za fedha hazitoi mkopo kwa watu ambao hawana dhamana ni kupoteza muda wako. Nikuulize wewe akija mtu yeyote akakuambia nipe elfu kumi nitakurudishia nikiipata utampa? Ni vigumu sana. Kwa kuwa ni vigumu kupata mkopo kwenye taasisi za fedha leo JIONGEZE na sehemu hizi tano ambazo unaweza kupata mtaji wa kuanzia biashara.

1. Akiba zako mwenyewe.

Kama huna kazi ya kukupatia kipato tafuta hata kazi ya kibarua, ifanye na weka akibakatika kila unachopata, baada ya muda tumia akiba hii kuanza biashara.

2. Michango kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki.

Unaweza kukusanya mchango kutoka kwa ndugu jamaa na hata marafiki. Wape wazo lako na omba wakuchangie.

3. Kuanza na biashara ambayo haihitaji mtaji.

Kuna biashara nyingi ambazo unaweza kuanza bila ya mtaji. Anza na biashara hizi na ukishaanza kupata kipato kikubwa unaweza kuhamia kwenye biashara unayoitaka.

SOMA; Biashara tano unazoweza kuanza kufanya bila mtaji.

4. Kuandaa wazo zuri.

Kama una wazo zuri sana ambalo linaweza kufanyika ila huna mtaji, liandae wazo hilo vizuri sana na kisha angalia kampuni ambazo zinaweza kufaidika na wazo hilo kisha wauzie wazo hilo au wakupe sehemu ya faida itakayopatikana kwa wazo lako.

ANGALIZO; Sajili wazo lako kwenye mamlaka husika(BRELA) ili usije ukaibiwa wazo hilo.

5. Shiriki mashindano mbalimbali.

Kuna mashindano mengi sana yanafanyika siku hizi ambayo yanapambanisha mawazo bora ya kibiashara. Andaa wazo lako na ingia kwenye mashindano haya. Ukiweka wazo lako vizuri unaweza kuwa mshindi na ukapata mtaji.

Tumia njia hizo tano kupata mtaji wa kuanzia biashara. Kama unaona njia hizi hazifai au haziwezekani kwako endelea kukaa nyumbani na kuperuzi mitandao ya kijamii huku ukiendelea kupoteza muda.

Amua sasa kubadili maisha yako, chukua hatua.

0 comments: