Mambo Matano(5) Ya Kufanya Siku Ya Jumatatu Ili Kuwa na Wiki Yenye Mafanikio.

Jumatatu ndio siku inayochukiwa na watu wengi kuliko siku nyingine yoyote ya wiki. Siku hii imepewa majina mabaya sana likiwemo BLUE MONDAY.

Jumatatu ni siku ambayo watu wanatoka kwenye mapumziko na kuanza tena kazi. Ni siku ambayo watu wanajua kuna siku tano za kazi mbele, na kama hupendi kazi yako ndio unazidi kupata msongo wa mawazo.

Leo JIONGEZE na mambo haya matano ambayo ukiyafanya siku ya jumatatu utakuwa na wiki yenye mafanikio makubwa.

1. Amka mapema na fanya mazoezi.

Kama mwishoni mwa wiki ulipumzika au kustareheka sana, jumatatu amka mapema na fanya mazoezi. Itakuwezesha kuianza wiki vizuri. Pia tumia muda huo wa asubuhi kupitia malengo na mipango yako ya wiki nzima.

Soma; faida 5 za kukimbia dakika 5 kila siku 

2. Pata kifungua kinywa.

Watu wengi sana hukosa muda wa kupata kifungua kinywa hivyo kuianza siku yao wakiwa wamechoka. Pata kifungua kinywa ili uianze wiki yako ukiwa na nguvu za kutosha.

3. Wahi kazini au kwenye biashara zako.

Tafiti zinaonesha jumatatu ndio siku ambayo watu wengi wanachelewa au kutokuhudhuria kabisa kazini au kwenye biashara zao. Sasa wewe usiwe mmoja wao, fika eneo lako la kazi mapema.

4. Jiandae kwa mambo usiyotegemea.

Kama umeajiriwa jumatatu unaweza kukutana na mabadiliko mengi sana kwenye eneo lako la kazi. Unaweza kukuta jukumu ulilokuwa unafanya unatakiwa uache na kukamilisha lingine lenye uhitaji wa haraka. Hata kama umejiajiri kutakuwa na mabadiliko ya hapa na pale tofauti na ulivyotegemea.

5. Kumbuka kuna jumanne.

Jumatatu inaweza kuwa siku ngumu sana kwako. Unajikuta na majukumu mengi na huku ukiwa haupo kwenye hali nzuri ya kufanya kazi. Usijiumize sana pale unaposhindwa kumaliza yote, kwa sababu sio mwisho wa dunia, kuna jumanne. Fanya kwa uwezo wako na endelea siku ya jumanne.

Naamini haya matano yataifanya jumatatu na wiki yako kuwa ya mafanikio.

Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.

0 comments: