Mambo 10 Unayotakiwa Kujua Kuhusu Uwekezaji.

Moja ya njia za kuelekea kwenye utajiri ni kuwa mwekezaji. Unapokuwa mwajiriwa unawasaidia wengine kuwa matajiri. Unapojiajiri au kufanya biashara unaanza kujijengea utajiri. Unapokuwa mwekezaji unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kufikia utajiri.

Hivyo ni muhimu sana wewe kuwa mwekezaji. Ila kabla hujawa mwekezaji, JIONGEZE na mambo haya kumi muhimu unayotakiwa kujua kuhusu uwekezaji.

1. Akiba uliyoweka benki sio uwekezaji. Hela iliyoko benki inazalisha kiasi kidogo sana na wakiondoa makato ni kama hakuna unachopata. Hata ukiwa na nyingi kiasi gani benki, sio uwekezaji.

2. Uwekezaji ndio njia pekee ya kuenda na mfumuko wa bei. Ukiweka hela benki, inapungua thamani kutokana na mfumuko wa bei. Ukiwekeza hela thamani yake inaongezeka jinsi mfumuko wa bei unavoongezeka.

3. Uwekezaji ni hatari. Kupitia uwekezaji unaweza kutengeneza fedha nyingi na pia unaweza kupoteza fedha nyingi.

4. Kununua hisa ni kumiliki kampuni. Unaponunua hisa za kampuni fulani unakuwa unamiliki sehemu ya kampuni hiyo. Ikipata faida na wewe unapata na ikipata hasara na wewe unapata.

5. Vipande ni kukopesha fedha. Unaponunua vipande ni kama umeikopesha taasisi fedha na hivyo kuweza kuitumia kwenye shughuli nyingine za kibiashara. Baadae unapata faida kutokana na vipande vyako.

6. Kuanza mapema ni faida kubwa. Kama utaanza kuwekeza ukiwa na umri mdogo ukifikia uzeeni utakuwa umefaidika sana na umejifunza sana.

7. Uwekezaji maarufu sio mzuri kwako. Kitu ambacho ni maarufu sana na ambacho kila mtu anawekeza hakina faida kubwa.

8. Usiwekeze fedha utakayoihitaji karibuni. Uwekezaji una changamoto nyingi sana na kama thamani imeshuka sana ukisubiri itapanda tena. Kama unawekeza fedha ambayo unatarajia kuitoa huwezi kunufaika.

9. Hakuna awezaye kutabiri soko la kesho. Ni vigumu sana kuweza kutabiri ni nini kitatokea siku zijazo, lakini unaweza kujipanga vizuri.

10. Unahitaji kujifunza kila siku kuhusu uwekezaji na mbinu mbali mbali za mafanikio kwenye uwekezaji. Soma kitabu THE INTELIGENT INVESTOR, utajifunza mengi.

Anza sasa kuwekeza au kuweka mipango ya kuwekeza. Jinsi utakavyoanza mapema ndivyo utakavyonufaika zaidi. Kwa hapa tanzania unaweza kuwekeza kwa kununua hisa, kununua vipande vya UTT, kununua ardhi, Kujenga nyumba za kuuza na kupangisha na hata kununua kampuni au biashara.

Nakutakia kila la kheri, TUPO PAMOJA.

0 comments: