Dalili Kumi Kwamba Tayari Wewe Ni Kiongozi.
Kwenye makala zilizopita tumeona ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuwa kiongozi. Pamoja na umuhimu huo sio watu wote ni viongozi na sio watu wote wataweza kuwa viongozi. Na hata ambao ni viongozi sio wote ni viongozi bora wanaotoa matokeo mazuri.
Pia tumejifunza kwamba kiongozi anaweza kuzaliwa au kutengenezwa. Kutegemea na mazingira na uhitaji wa mtu, mtu yeyote anaweza kuendeleza tabia za uongozi ndani yake.
Leo tutaona dalili kumi za sifa ya uongozi. Kama wewe una sifa hizi tayari wewe ni kiongozi na unahitaji kujiendeleza zaidi ili kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye uongozi wako. Kama huna dalili hizi kuna habari nzuri na mbaya kwako.
Habari mbaya kwako ni kwamba utaendelea kuwa mfuasi maisha yako yote na kwa nafasi kubwa utashindwa kuonesha uwezo wako wa kweli na kuleta tofauti kubwa kwenye jamii yako na dunia kwa ujumla.
Habari nzuri ni kwamba unaweza kujifunza tabia hizi na ukawa kiongozi bora sana. Uzuri ni kwamba kila kitu unaweza kujifunza, ni utayari wako na juhudi zako ndivyo vitakufanya uweze kujua kile unachotaka kujua. Njia bora ya kujifunza uongozi ni kujua vitu na kuvifanyia kazi. Hutakuwa kiongozi kwa kusoma tu hapa, bali soma na utumie yale unayojifunza kwenye maisha yako ya kila siku.
Kwa kifupi sana naomba nitaje dalili kumi zinazoonesha kwamba wewe ni kiongozi. Kwa maelezo zaidi tunaweza kujadiliana kwenye maoni hapo chini.
1. Unapenda kuleta mabadiliko.
2. Una ndoto kubwa sana mpaka wengine wanaona haziwezekani.
3. Husubiri kuambiwa nini cha kufanya,
4. Unapenda kutatua matatizo yanayowasumbua wengine.
5. Hupendi kulalamika au kulaumu wengine.
6. Unajali sana na kukuza mahusiano.
7. Matendo yako na maneno yako vinaendana.
8. Hukubaliani na mifumo isiyo na tija.
9. Uko tayari kukiri makosa na kuomba radhi.
10. Unapenda kujifunza mambo mapya na kuhusu uongozi.
Kama una dalili hizo kumi hongera wewe ni kiongozi. Kama huna usikate tamaa bado una nafasi kubwa ya kujijengea uongozi.
Uongozi unaanza na kuchagua kuwa kiongozi, baada ya hapo unaendelea kujifunza na kupata uzoefu. Karibu kwenye mafunzo ya kuongozi kupitia blog hii. Ili kuhakikisha hukosi mafunzo haya weka email yako hapo juu kwenye blog ili upate makala hizi moja kwa moja kwenye email yako.
TUKO PAMOJA.
4/20/2014 07:04:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Makosa Makubwa Matano Yanayoweza Kukuharibu Wewe Kama Kiongozi.
Ili uweze kufanikiwa kwenye uongozi kuna mambo muhimu unatakiwa kuwa unafanya na pia kuna mambo mengine unatakiwa kuepuka kufanya.
Katika makala zilizopita tumekuwa tukiangalia mambo muhimu ya kufanya ili kuweza kufanikiwa kwenye uongozi. Ili kuwa kiongozi mzuri ni muhimu kuwa na maono, ushawishi, ushirikiano na uadilifu. Kuwa na mpango mikubwa na kuweza kuwashawishi wengine kuifikia ili kuboresha maisha yako ni tabia moja inayoweza kukutengeneza kuwa kiongozi bora.
Pamoja na hayo kuna mambo ukiyafanya unaweza kuharibu sana uongozi wako bila ya kujali umeutengeneza kwa muda gani. Mambo haya yamekuwa yakifanywa na watu wengi na ndio sababu kubwa ya wao kushindwa kuwa viongozi wazuri. Kwa kuwa wewe unajifunza kuwa kiongozi bora, ni muhimu sana ukayajua mambo haya ili usije kuyafanya na ikakugharimu kwenye maisha yako na uongozi wako.
Hapa nitaongelea makosa kubwa matano unayoweza kufanya yakaharibu kabisa uongozi wako. Makosa hayo ni kama ifuatavyo.
1. Kutaka kupendwa badala ya kuheshimika.
Ni rahisi sana kwa kiongozi kutaka watu wampende yeye kutokana na uongozi wake. Ili kutimiza hilo anajikuta anafanya mambo ya kuwafurahisha watu badala ya kufanya mambo yatakayowasaidia watu. Katika uongozi kuna maamuzi unaweza kufanya watu wasikuelewe kwa sababu wewe una maono, baadae mafanikio yanapoonekana watu hukuheshimu sana kama kiongozi. Ila ukitaka kuwafurahisha watu hutoweza kufanya mambo ya kuwasaidia. Usitake kupendwa na watu bali jenga kuheshimiwa na watu kutokana na maamuzi unayofanya yenye manufaa kwenye maisha yao.
2. Kutochukua ushauri na msaada wa wengine.
Kuna wakati kiongozi anaweza kuona yeye yupo juu ya wengine hivyo ushauri wake ndio sahihi. Pia anafikiri hahitaji msaada wowote kutoka kwa anaowaongoza. Hili ni kosa kubwa sana unaloweza kufanya wewe kama kiongozi. Bila ya kujali ngazi yako ya uongozi ni muhimu sana kuchukua ushauri kwa unaowaongoza. Wakati mwingine kuna mawazo mazuri sana kutoka kwa unaowaongoza, pia unaweza kupata msaada mkubwa kutoka kwa unaowaongoza.
3. Kutokujali na kuendeleza vipaji vya wengine.
Watu unaowaongoza wana vipaji na uwezo mkubwa sana. Kazi yako kama kiongozi ni kuendeleza vipaji hivi ili kuwawezesha kufikia malengo makubwa kwenye maisha yao. Kama kiongozi hutothamini vipaji na uwezo wa watu wako itakuwa vigumu sana kwao kukufuata na hii itaathiri uongozi wako.
4. Kushindwa kupanga majukumu vizuri kwa unaowaongoza.
Kama wewe ni kiongozi wa timu au kikundi ambacho kinatakiwa kukamilisha jukumu fulani ni muhimu sana kila mtu kujua jukumu lake ni nini na anawezaje kulitimiza. Kushindwa kupanga na kueleza vizuri majukumu ya kila mtu ni chanzo kikubwa cha kupungua kwa uzalishaji kwenye maeneo mengi ya kazi. Wewe kama kiongozi hakikisha wafuasi wako wanajua majukumu yao na njia za kuyatimiza.
5. Kushindwa kutoa taarifa kwa watu.
Ni muhimu sana kutoa taarifa kwa wale unaowaongoza. Watu wanataka kujua ni mafanikio kiasi gani yamefikiwa na ni changamoto gani zinawarudisha nyuma. Wewe kama kiongozi unajukumu la kutoa taarifa sahihi na kwa muda sahihi kwa watu unaowaongoza. Hii itawafanya kuwa sehemu ya uongozi wako na kuufurahia.
Kama ukiweza kuepuka mambo haya matano, utafanikiwa sana kwenye uongozi wako. Kumbuka ni muhimu sana kwako kuwa kiongozi kwenye maisha yako. Na unaweza kujifunza kuwa kiongozi bora. Weka email yako hapo juu(kwenye blog) ili kupata makala hizi za mafunzo ya uongozi moja kwa moja kwenye email yako.
Karibu sana.
4/13/2014 10:16:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Siri Kumi za Mafanikio Kwenye Uongozi.
Katika watu wengi wanaopewa nafasi za kuongoza kuna wachache sana ambao wanakuwa ni viongozi bora. Wengine wanaishia kuwa tu na majina ya uongozi ila wanashindwa kufanya mambo makubwa kupitia nafasi zao za uongozi.
Mpaka unasoma hapa naamini unataka kuwa kiongozi bora. Ili uweze kupata mafanikio kwenye uongozi, kuna tabia kumi muhimu unatakiwa kuwa nazo na kuziendeleza. Tabia hizo ziko wazi kabisa ila kutokana na watu wengi kutozipa mkazo zimegeuka na kuwa siri kubwa.
Leo tutazungumzia tabia kumi muhimu za kufanikiwa kwenye uongozi. Tabia hizi zinafanya kazi bila ya kujali wewe ni kiongozi wa aina gani. Uwe ni kiongozi usiyekuwa na cheo, kiongozi wa wananchi, kiongozi wa shughuli zako au hata kiongozi wa maisha yako ni vyema ukaanza kutengeneza na kuendeleza tabia hizi.
1. Mfano.
Ili uweze kufanikiwa kama kiongozi ni lazima uwe mfano bora kwa wale unaowaongoza. Utatengeneza mfano mzuri pale ambapo utakuwa unatenda yale unayohubiri. Lazima wewe uwe wa kwanza kuonesha mwendo ili wafuasi wako nao wafuate. Ile kauli kwamba “fuata maneno yangu, usifuate matendo yangu” imesababisha watu wengi sana kushindwa kwenye uongozi. Watu wanapenda kumfuata na kumheshimu mtu ambae anaonesha mfano wa vitendo kwao.
2. Nguvu,
Mafanikio katika uongozi yanategemea sana nguvu ya kiongozi. Naposema nguvu simaanishi nguvu za kimwili pekee bali hata nguvu za kihisia, nguvu za kiakili na nguvu za kiimani. Kiongozi unapokuwa na nguvu hizi inakuwa rahisi kuzitoa kwa wale unaowaongoza.
3. Shauku.
Viongozi wanaofanikiwa sana ni wale wenye shauku kubwa kwenye kazi zao na kwenye maendeleo ya watu wanaowaongoza. Kwa kuwa na shauku kunawafanya wafanye mambo bora zaidi. Pia shauku inaambukizwa mpaka kwa wafuasi.
4. Uvumilivu.
Bila ya uvumilivu huwezi kuwa kiongozi bora, hakuna zaidi ya hapo. Viongozi wengi waliofanikiwa sana walipitia mambo magumu sana kwenye maisha yao. Hata wewe utapitia mambo magumu sana kwenye uongozi wako na maisha yako kwa ujumla. Kuna wakati utashindwa, kuna wakati utakosea sana, tumia nyakati hizi ngumu kujijenga na kuwa imara. Unapovumilia na kuvuka nyakati hizi ngumu unatoa imani kubwa kwa wafuasi wako.
5. Uelewa wa kihisia.
Hisia ni moja ya vitu vinavyoweza kumjenga kiongozi au kumbomoa ndani ya muda mfupi sana. Ili kuwa kiongozi bora ni lazima uzijue hisia zako na ujue ni jinsi gani ya kuzimiliki. Usikubali hisia zako zikutawale mwishowe uanze kufanya mambo yatakayoharibu sifa zako. Pia ni muhimu kuweza kusikiliza na kuelewa hisia za wafuasi wako na kuweza kuwasaidia kupata mtazamo sahihi.
6. Uwezeshaji.
Kiongozi bora ni yule anayewawezesha wafuasi wake kuchukua hatua na kufanya mabadiliko kwenye kazi zao na maisha yao. Katika uwezeshaji kiongozi anawapa watu nguvu na mamlaka ya kufanya mambo ambayo yatakuwa na manufaa kwenye maisha yao. Unapowawezesha watu kuchukua hatua, unawajengea ujasiri ambao baadae utawapelekea kuwa viongozi bora.
7. Ufanisi.
Viongozi bora huwa na ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yao. Katika ufanisi viongozi huwa na mipango mizuri ambayo itawasaidia kufikia malengo waliyojiwekea. Viongozi bora hufanya jambo sahihi na sio kufanya jambo kwa usahihi. Uongozi bora unapimwa kutokana na majibu anayozalisha kiongozi na sio kwa hotuba nzuri.
8. Kuchukua hatua.
Viongozi bora wanajua ni wapi walipo na pia wanajua ni wapi wanataka kwenda na huchukua hatua mara moja ili kufika wanakotaka kwenda. Hapa ndipo viongozi wanapobadili maono kuwa uhalisia. Kama kiongozi una ahadi na maneno mengi mazuri ila huwezi kuchukua hatua ya kuyatekeleza hufai kuwa kiongozi bali muigizaji.
9. Mafanikio.
Mafanikio ni nguzo muhimu sana kwa viongozi waliofanikiwa. Kiongozi lazima awe amefanikiwa kwenye shughuli zake ili aweze kupata wafuasi wanaotaka kufanikiwa kama yeye. Viongozi bora hupanga kuwa bora kwenye shughuli zao na hivyo kukazana kila siku kutoa majibu yenye ubora.
10. Maadili.
Tabia hii imekuja mwisho ila ilipaswa kuwa ya kwanza kabisa. Huwezi kufanikiwa kwenye uongozi wa aina yeyote ile kama huna maadili. Watu wanapenda kumfuata mtu ambaye anajiheshimu na hivyo kuamini atawaheshimu. Kama kiongozi una skendo chafu ni vigumu sana watu kukupa imani ya kweli kutoka ndani ya mioyo yao. Tatizo kubwa tunalolipata kwenye uongozi hapa Tanzania ni maadili mabovu ya viongozi. Kuwa kiongozi wa mfano kwa kuwa na maadili mazuri kwenye maisha yako.
Kwa kujijengea na kuendeleza sifa hizo kumi utajijenga kama kiongozi wa mfano na mwenye mafanikio makubwa sana. Kumbuka wewe ni kiongozi, hivyo endeleza uongozi wako ili uweze kuwasaidia watu wengi zaidi.
Kama una jambo lolote unaona ni zuri kutushirikisha tafadhali weka maoni yako hapo chini. Kwa kuweka maoni yako hapo chini ni dalili nzuri kwamba unaelekea kuwa kiongozi bora na wa mfano.
Karibu kiongozi tujadiliane yaliyo mema kwenye uongozi.
4/06/2014 07:11:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Huhitaji Cheo Ili Kuwa Kiongozi.
Ni wakati gani unafikiri unahitaji kuanza kuonesha tabia za uongozi? Unapoambiwa umepewa nafasi ya kuwa meneja? Au unapoteuliwa kuwa mwakilishi wa watu au msimamizi wa sekta fulani? Yote hayo yanaweza kukupa nguvu ya uongozi ila hayawezi kukufanya kiongozi kama hukuwa kiongozi kabla. Na vibaya zaidi ni kwamba nguvu hii ya uongozi huisha mara moja pale nafasi hiyo inapoondoka.
Huhitaji cheo ili kuwa kiongozi, unahitaji kutumia uwezo wako na vipaji vyako katika maisha yako ili kuwa kiongozi. Unahitaji kutimiza wajibu wako na kufanya zaidi ya unavyotegemewa kwenye kazi, biashara na hata kwenye maisha yako. Kwa kufanya hivi ndio utajitengeneza kama kiongozi ambapo wengine watafurahia kukufuata.
Ili kuwa kiongozi huhitaji cheo, unahitaji kufanya maamuzi ya kuwa kiongozi kisha kuanza kuongoza. Kila mtu anayo nafasi ya kuwa kiongozi ila wachache ndio wanaochagua kuwa viongozi. Kama kila mtu angefagia mtaa wake dunia nzima ingekuwa safi sana. Ila kwa kuwa wengi hawafanyi wanayopaswa kufanya tunaishia kuwa na matatizo mengi duniani.
Nguvu nne za uongozi ambazo hazihitaji cheo.
Kama unajiuliza unawezaje kuwa kiongozi bila ya kuwa na cheo soma nguvu hizi nne za uongozi ambazo tayari unazo bila hata ya kuwa na cheo. Kwa kufanya mambo haya manne ambayo hayahitaji cheo kutakutengeneza kuwa kiongozi mzuri kwenye maisha yako.
1. Una uwezo wa kwenda kwenye shughuli zako, iwe kazi au biashara na kufanya kazi kwa moyo mmoja na ubunifu wa kipekee kitu ambacho kitakufanya utoe majibu mazuri sana. Una uwezo wa kuamua kuwa bora siku ya leo zaidi ya ulivyokuwa bora siku ya jana na huhitaji kuwa na cheo ili kufanya hivyo. Kwa kutimiza wajibu wako na kuongeza ubora kila siku unakuwa kiongozi ambaye wengine watapenda kukufuata.
2. Leo hii unao uwezo wa kushawishi na kuchochea watu wanaokuzunguka ili wafanye mambo ambayo yatawasaidia kuboresha kazi zao na maisha yao kwa ujumla. Huhitaji kuwa na cheo ndio uweze kumshawishi mtu kwamba akifanya juhudi kwenye kazi zake ataboresha maisha yake. Unahitaji kumuonesha picha kubwa na kumchochea aweze kuifikia, kama na wewe unaelekea kuifikia au umeshaifikia.
3. Unao uwezo wa kuleta mageuzi chanya kwenye mazingira hasi. Hata mazingira ya kazi au maisha yawe magumu kiasi gani unao uwezo wa kubadili mtazamo wako na wa wanaokuzunguka kuhusu mazingira hayo. Huhitaji cheo kuweza kuangalia faida unayoweza kupata kwenye mazingira fulani zaidi ya kuangalia hasara tu. Pia huhitaji cheo kubadili mazingira mambovu ambayo yanakukandamiza wewe au wale wanaokuzunguka.
4. Una uwezo wa kuwa mwema kwa wale wanaokuzunguka kwenye shughuli zako na maisha yako kwa ujumla. Huhitaji cheo ndio uweze kuwaheshimu, kuwajali na kuwapenda watu wanaokuzunguka kwenye maisha yako. Kwa kufanya hivyo utawafanya watu hawa kufurahia kuwa karibu na wewe na kuona maisha yao yana thamani kubwa. Mtu anayeona thamani kubwa ya maisha yake anaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yake na shughuli zake.
Mambo haya manne hayahitaji cheo ndio uweze kuyafanya. Hebu anza kuyafanya mara moja kwenye maisha yako na utaona mabadiliko makubwa. Kumbuka wewe ni kiongozi hata kama huna cheo.
3/30/2014 07:55:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Je Wewe ni Kiongozi au Mfuasi?
Duniani tuna makundi mawili ya watu, kuna kundi la kwanza ambapo watu hawa ni viongozi na kundi la pili ambapo watu hao ni wafuasi. Mara nyingi wanaofanikiwa sana na kufikia malengo waliyojiwekea ni wale waliopo kwenye kundi la viongozi.
Viongozi huanzisha na wafuasi hufuata au kuiga, hii ndio inawafanya viongozi wanafanikiwa sana kwenye mipango yao. Hakuna mtu anayepanga huyu awe kuingozi na huyu awe mfuasi. Ni mfumo wako wa maisha na tabia zako zitakuweka kwenye kundi la viongozi au kundi la wafuasi.
Je unajua wewe upo kwenye kundi gani? Unaweza kujiita kiongozi kwa kuwa umepewa nafasi ya kuwasimamia watu, ila kama huna sifa za uongozi basi wewe sio kiongozi bali ni msimamizi tu. Hapa tutaangalia tofauti tano za kitabia kati ya viongozi na wafuasi. Kwa kuzijua tofauti hizi za kitabia itakufanya ujue upo kundi gani na pia uweze kuchukua hatua.
1. Uanzilishi.
Viongozi huanzisha mambo kutokana na malengo na mipango yao kwenye maisha na kazi wanazofanya. Hujua ni nini watafanya kwenye kila hatua na mwishowe hufanikiwa.
Wafuasi hufanya mambo yaliyoanzishwa na watu wengine. Hata siku moja hawana udhubutu wa kuanzisha kitu chao wenyewe na kukisimamia mpaka kitoe majibu wanayotarajia. Wafuasi huishia kuiga mambo yanayofanywa na watu wengine na inakuwa rahisi kwao kushindwa.
2. Mawasiliano.
Viongozi huanzisha mawasiliano na watu wengine. Mara nyingi huwa wa kwanza kuwatafuta watu wanaowahitaji ili kukamilisha jambo fulani. Pia huwa wa kwanza kuwapigia wengine simu katika kuwasiliana.
Wafuasi huwa ni wasikilizaji kwenye mawasiliano. Ni wazuri kupokea taarifa walizopewa na kwenda kuzifanyia kazi. Kama wasipotafutwa hawajisumbui kutafuta mtu, hukaa na kusubiri. Wafusi husubiri simu iite wapewe taarifa au maagizo.
3. Matumizi ya muda.
Viongozi hutumia sehemu kubwa ya muda wao kupanga mipango mbalimbali. Pia hutumia muda huo kufikiri matatizo yanayoweza kutokea na kufikiri njia za kukabiliana nayo. Kwa njia hii viongozi wanaongeza uwezo wao wa kutatua matatizo.
Wafuasi hutumia muda wao mwingi kuishi maisha yao ya kawaida na hawana muda mwingi wa kuweka mipango mikubwa. Wafuasi ni wazuri kustushwa pale tatizo linapotokea na huwa wa kwanza kusumbuliwa na tatizo hilo. Kibaya zaidi wanakuwa hawana uwezo wa kutatua tatizo hilo zaidi ya kupata msongo wa mawazo.
4. Uwekezaji wa muda.
Viongozi huwekeza muda wao kwa watu wengine. Hutumia muda wao mwingi kujenga na kufundisha watu kuwa viongozi. Pia hutumia muda kuwapa wengine uwezo wa kuweka mipango na kutatua matatizo.
Wafuasi hawawekezi muda wao bali wanautumia na watu wengine. Wafuasi wanapokuwa na muda wa ziada huutumia kufanya mambo ambayo hayana msaada wowote kwao kimaisha au kikazi. Ni watumiaji wa muda hovyo.
5. Upangaji wa ratiba.
Viongozi wanapanga ratiba zao kulingana na vipaumbele vyao. Hupanga ratiba kutokana na malengo na mipango yao na huweka mbele vipaumbele vyao.
Wafuasi hupanga ratiba zao kulingana na maombi na maagizo. Ratiba za wafuasi zimejaa vitu ambavyo ni maombi ya watu wengine au ni maagizo ya watu wengine. Hawawezi kuweka vipaumbele vyao wenyewe kwenye ratiba zao.
Hizo ndio tofauti tano kati ya viongozi na wafuasi kitabia. Hakuna mtu anayekupangia tabia hizi bali unaziendeleza mwenyewe.
Kama kwa tabia hizo hapo chini unajiona uko upande wa wafuasi usife moyo. Kama tulivyosema, viongozi pia hutengenezwa, hivyo unaweza kujitengeneza kuwa kiongozi mzuri na ukafanikiwa kwenye mipango yako ya maisha. Jiunge na mtandao huu kwa kuweka email yako hapo juu kwenye blog ili kupata mafundisho haya ya uongozi moja kwa moja.
Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za maisha, kumbuka viongozi ndio wanaofanikiwa kwenye nyanja yoyote.
3/23/2014 10:18:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Sifa Moja Muhimu Ambayo Kila Kiongozi Mkubwa Anayo.
Kwenye makala zilizopita tuliona ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuwa kiongozi kwenye maisha yake na shughuli anazofanya. Pia tuliona kwamba kila mmoja wetu anaweza kuwa kiongozi kama ataamua, iwe kwa kuendeleza sifa za uongozi zilizopo ndani yake au kwa kujifunza sifa za uongozi.
Leo tutaangalia sifa moja muhimu ambayo kila kiongozi mkubwa anayo na imechangia sana kwenye mafanikio yao kiuongozi. Ninaposema viongozi wakubwa simaanishi viongozi walioshika nafasi kubwa bali viongozi ambao wamefanya mambo makubwa ambayo yameleta mabadiliko kwa watu wengi na dunia kwa ujumla. Viongozi kama Nyerere, Mandela na hata viongozi wakubwa kwenye nyanja za biashara na kazi wameweza kufikia mafanikio makubwa kutokana na sifa hii moja.
Kwa kuwa na wewe unataka kuwa kiongozi wa maisha yako, kiongozi kwenye familia yako, kiongozi kwenye kazi au biashara zako na hata kiongozi wa kuwakilisha watu ni vyema ukaijua sifa hii na kuanza kujifunza au kuiendeleza ili uweze kufikia malengo yako. Sifa hii moja sio kwamba ndio inakutosha kuwa kiongozi ila kwa kuwa na sifa hii unaweza kuziendeleza sifa nyingine za uongozi. Kwa kukosa sifa hii ni vigumu kuweza kuzitumia sifa nyingine za uongozi ulizonazo.
Sifa muhimu ya uongozi ninayozungumzia hapa ni ujasiri. Ujasiri ni sifa ambayo imewawezesha viongozi wakubwa kufanya mambo makubwa kwenye uongozi wao. Kukosa ujasiri ndio kumefanya watu wengi washindwe kwenye uongozi.
Kuweza kusimamia kile unachoamini ni sahihi hata kama watu wengi wanakupinga kunahitaji ujasiri wa hali ya juu. Kama ilivyotokea kwa Mandela, alikuwa na ujasiri wa kuweza kusimama na kupinga ubaguzi hata baada ya kufungwa jela miaka 27. Wafanyabiashara wakubwa na waliofanikiwa sana mwanzoni walipingwa, kukatishwa tamaa na hata kuchekwa kwamba mawazo yao ya biashara hayawezi kufanikiwa. Ila kutokana na ujasiri waliweza kuendelea na misimamo yao na baadae ikawa historia kubwa ya mabadiliko.
Inahitaji ujasiri wa hali ya juu kuenda tofauti na watu wengine ili kufuata ndoto zako. Inahitaji ujasiri mkubwa kuweza kufanya kazi na watu ambao wana misimamo tofauti na wewe na mkaweza kuelewana. Inahitaji ujasiri mkubwa kufanya na kusimamia maamuzi magumu ambayo wengi hawayafurahii ila yana manufaa kwao baadae. Yote haya yameweza kutengeneza viongozi wakubwa sana na walioshindwa ujasiri wa kufanya mambo haya wameishia kuwa kawaida tu.
Kutokukata tamaa wakati umeshindwa, kuweza kusimama baada ya kupata hasara kubwa na kutokuwasikiliza wanaokukatisha tamaa ni muhimu sana kwenye mafanikio ya kibiashara na kikazi. Watu wenye ujasiri wanaweza kuvuka changamoto hizo na kuwa viongozi wa mfano kwenye kazi na biashara zao.
Unaweza kujifunza ujasiri?
Huenda mpaka kufika hapa umeshaona kwamba ujasiri kwako ni kitu kigumu sana hivyo njia yako ya kuwa kiongozi imeshakutana na kizuizi kikubwa. Habari njema kwako ni kwamba unaweza kujifunza ujasiri. Unawezaje kujifunza ujasiri?
Ili uwe na ujasiri kitu cha kwanza kabisa ni lazima ujue ni nini unasimamia. Kama huna kitu unachosimamia utakubaliana na kila kitu na kama unakubaliana na kila kitu wewe sio jasiri na huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote unalofanya, hilo halina ubishi. Jua ni kitu gani unasimamia, jua ni kwa nini unasimamia na jua ni nini unategemea kutoka kwenye huo msimamo wako. Hii ni kwenye maisha, familia, kazi, biashara na hata uongozi wa wananchi.
Baada ya kujua unachosimamia izidi hofu. Hofu na woga ndio vitu vinavyoondoa ujasiri kwa watu wengi. Ukiweza kuishinda hofu utaweza kukamilisha mambo mengi sana kwenye maisha yako na kuacha alama. Kama utakubaliana na hofu na kuacha kufanya mipango yako hakuna kitu kikubwa utakachofanya. Watu wenye ujasiri na waliofanikiwa sio kwamba hawana hofu ila wamechagua kuzishinda hofu zao. Chagua na wewe kushinda hofu zako na kufanya yale unayojua ni sahihi na yatawasaidia watu wengine.
Kuna faida kubwa ya kuwa na ujasiri kwenye maisha yako. Watu wenye ujasiri huwavutia watu wengine kuwa karibu nao na hivyo kuangaliwa kama kiongozi. Watu wenye ujasiri hufanya mambo makubwa na kuwafaidisha wengine hivyo wengine kutaka kufanya kama wao. Hivi ndivyo ujasiri unajenga viongozi wakubwa. Na kwa kuwa wewe unataka kuwa kiongozi mkubwa anza kwa kujenga ujasiri wako.
Kwanzia wiki ijayo tutazijadili sifa 21 za kiongozi kutoka kwenye kitabu The 21 Indispensable Qualities of a Leader. Tutajadili sifa tatu tatu mpaka zitakapoisha. Kuhakikisha hukosi makala hizi nzuri za uongozi weka email yako hapo juu kwenye blog sehemu iliyoandikwa jiunge hapa kupata makala mpya inapotoka
Pia usiache kupitia blog hii kila jumapili ili kujifunza mengi kuhusiana na uongozi. Washirikishe marafiki zako nao ili wajifunze masomo haya ya uongozi. Pia weka maoni yako hapo chini kuhusiana na mambo ya uongozi.
3/16/2014 11:44:00 AM | Labels: UONGOZI | 0 Comments
Kiongozi Anazaliwa au Anatengenezwa? Jibu Hili Hapa.
Kumekuwa na mjadala au mabishano kwa muda mrefu ikiwa kiongozi anazaliwa au anatengenezwa. Wapo wengi ambao wanaamini watu wenye sifa za uongozi wanazaliwa nazo na haziwezi kutengenezwa. Wapo wengine wanaoamini viongozi wanatengenezwa kutokana na jamii wanayoishi na elimu wanayopata.
Nani yupo sahihi hapa? Je wewe una maoni gani juu ya tabia za uongozi? Je mtu anazaliwa nazo au anazipata kutoka kwenye malezi na elimu?
Majibu yote mawili ya kiongozi kuzaliwa au kutengenezwa yapo sahihi kabisa. Ni kweli kwamba kuna watu wanazaliwa wakiwa na sifa za uongozi na kuna wengine wanajifunza uongozi kutokana na malezi na elimu wanayopata.
Kwa nini tuna upungufu mkubwa wa viongozi?
Pamoja na kwamba viongozi wanaweza kuzaliwa na wengine kutengenezwa bado tuna upungufu mkubwa sana wa viongozi kwenye jamii zetu. Hii inasababishwa na kwamba jamii haitengenezi viongozi. Hivyo viongozi pekee wanaopatikana ni wale waliozaliwa na sifa za uongozi na huwa ni wachache sana.
Mfumo wa maisha wa jamii nyingi hautengenezi viongozi. Watoto wanakuzwa bila ya kujengewa misingi ambayo inawasaidia kuweza kufanya maamuzi kama viongozi. Jamii nyingi zinalea watoto kwa kuwaepusha wasikutane na changamoto ambazo zinawafanya wafikiri zaidi. Kwa njia hii jamii sio tu kwamba haitengenezi viongozi bali inaua sifa za uongozi kwa baadhi ya watoto waliozaliwa nazo. Kwenye jamii kuna watu wengi sana ambao hawana sifa za uongozi, kwa kuwa watoto wanaiga tabia za wanaowazunguka ni rahisi sana kwao kufanana na wanajamii ambao hawana sifa za uongozi.
Kitu kingine kikubwa kinachoua uongozi ni mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu hasa kwa nchi yetu Tanzania haujakaa kutengeneza viongozi. Kwanzia darasa la kwanza mpaka elimu ya chuo mtoto anafundishwa kukazania vitu vichache ili kufaulu masomo. Hapewi nafasi ya kufikiri tofauti na kuibua na kupambana na changamoto. Pia mfumo wa elimu unajenga watu kuwa na ubinafsi na kufikiria maisha yao tu badala ya kufikiri na ya wale wanaomzunguka. Kwa njia hii mfumo wa elimu unashindwa kutengeneza viongozi na inaua sifa za uongozi kwa baadhi ya wenye nazo.
Hata wewe unaweza kuwa kiongozi.
Hata wewe unaweza kuwa kiongozi, iwe umezaliwa na sifa za uongozi ama hukuzaliwa nazo. Unaweza kufufua sifa za uongozi zilizokufa ndani yako au kujifunza sifa mpya za uongozi.
Kama nilivyosema kwenye makala iliyopita ni muhimu sana wewe kuwa kiongozi(kuisoma bonyeza hapa). Ni muhimu wewe kuwa kiongozi kwa sababu wote wanaofanikiwa kwenye chochote wanachofanya wanasifa za uongozi. Ili uweze kufanikiwa kwenye biashara, kazi, sanaa, michezo na hata uongozi wa kisiasa ni lazima uwe na sifa za uongozi. Hata kwenye malezi ya familia, wazazi wenye sifa za uongozi wanalea familia zao vizuri na kuwa na watoto wanaoweza kuendesha maisha yao vizuri.
Hata wewe unaweza kuwa kiongozi mzuri na ukafanikiwa sana kwenye shughuli zako. Unaweza kujifunza sifa na tabia za uongozi na ukaanza kuzitumia kwa mafanikio yako. Kuna vitabu na maandiko mengi sana yanayozungumzia uongozi. Unaweza kutafuta na kuanza kusoma, ila kama unaona huna muda wa kutosha unaweza kuwa unajifunza kupitia blog hii. Kila wiki kutakuwa na makala moja inayohusiana na uongozi hivyo unaweza kuwa unakuja kujifunza hapa. Pia ili kuhakikisha hukosi makala yoyote inayohusiana na uongozi au mengineyo weka jina na email yako hapo juu kwenye blog na utapata makala hizi moja kwa moja kwenye email yako.
Karibu tutengeneze viongozi wa kuliinua taifa letu kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo kwa ujumla. Hili ni jukumu letu sote.
3/09/2014 07:56:00 AM | Labels: UONGOZI | 1 Comments
Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Kiongozi.
Katika safari ya malengo yangu ya kuwa rais wa Tanzania ifikapo mwaka 2040 moja ya maandalizi makubwa ni kujenga sifa za uongozi ndani yangu. Katika kujenga sifa kwangu mimi namkaribisha yeyote anayetaka kujenga sifa za uongozi ndani yake tuwe pamoja kwenye safari hii.
Nani anatakiwa kuwa kiongozi?
Dunia ya sasa inahitaji viongozi zaidi ya kitu kingine chochote. Kila mtu anatakiwa kuwa kiongozi na kuwa na sifa ya uongozi ndani yake.
Watu wengi wakisikia neno KIONGOZI AU UONGOZI mawazo yao yanakwenda moja kwa moja kwenye mambo ya siasa au taasisi mbalimbali. Ni kweli kwamba tunahitaji viongozi kwenye nafasi za kisiasa ama nyinginezo lakini tunahitaji viongozi wengi zaidi ya hapo.
Uongozi ni mfumo wa maisha, uongozi ni uwezo wa kushawishi watu kuchukua hatua kwa faida yao wenyewe na uongozi ni uwezo wa kubadilisha maono kwenda kwenye uhalisia. Tabia zote hizi zinahitajika kwenye maisha yetu kuanzia kwenye familia, kazi, biashara na maendeleo.
Ili uweze kulea familia ambapo wanafamilia wanajiamini na kuweza kufanya maisha yao kuwa bora unahitaji kuwa kiongozi mzuri.
Ili uweze kufanikiwa kwenye kazi yoyote unayofanya iwe umejiajiri au umeajiriwa ni muhimu sana kutumia sifa za uongozi zilizopo ndani yako.
Ili uweze kufanikiwa kwenye biashara ni muhimu sana kuwa kiongozi. Kuweza kuanzisha biashara ndogo na ikakua mpaka kufikia kampuni kubwa sana ni lazima uwe kiongozi mwenye maono na ushawishi mkubwa.
Ni vigumu sana kufanikiwa kwenye dunia ya sasa kama huna sifa za uongozi ndani yako. Wote wanaofanya vizuri kwenye maisha, biashara, kazi na hata burudani ukiwafuatilia kwa karibu wamakuwa na sifa za uongozi ndani yao.
Tumekosa viongozi
Tumefika hapa tulipo kama taifa kwa sababu tumekosa viongozi wenye sifa za uongozi. Tumekosa viongozi kwenye nafasi za kisiasa na tumekosa viongozi kwenye kila nyanja ya maisha kuanzia ngazi ya familia mpaka kwenye biashara.
Wengi walioshikilia nafasi za kisiasa sio viongozi, wako pale kwa maslahi yao binafsi na hili limetugharimu sana mpaka sasa.
Tumekosa uongozi kwenye familia ndio maana sasa hivi maadili yanaporomoka kwa kasi kubwa sana. Tumekosa uongozi mzuri kwenye kazi na biashara ndio ndio maana watu wanaishia kuigana na kushindana mwishowe kupotezana
Tunahitaji viongozi wengi wenye sifa za uongozi ili tuweze kuendelea kama taifa.
Katika shughuli yoyote unayofanya unahusisha watu na ili uweze kufanya kazi vizuri na watu mbalimbali ambao wana mitazamo mbalimbali utafanikiwa endapo tu una sifa za uongozi. Tofauti na hapo kazi inaweza kuwa ngumu sana kwako.
Wewe unahitaji kuwa kiongozi kwenye sehemu yako ya kazi, unahitaji kuwa kiongozi kwenye biashara yako, unahitaji kuwa kiongozi kwenye familia yako na una jukumu la kutengeneza viongozi wengi zaidi kwa maendeleo ya taifa letu.
Kama upo tayari kuwa kiongozi jiunge nami kwenye safari hii na tujifunze na kuendeleza sifa za uongozi zilizopo ndani yetu. Weka jina lako na email yako hapo juu kwenye blog ili upate kila makala ya uongozi inapotoka moja kwa moja kwenye email yako.
Katika safari hii tutajifunza uongozi, sifa za viongozi, uongozi na maendeleo, uongozi na siasa na jinsi ya kufanya maamuzi mbalimbali kama kiongozi.
Tuache kulalamika sasa na tuwe sehemu ya suluhisho kwa kuanza kuchukua hatua.
3/02/2014 05:56:00 AM | Labels: UONGOZI | 1 Comments