Ukiacha Kuangalia Facebook Kila Mara Mambo Haya Matano Yatatokea.

Facebook ni mtandao mkubwa sana wa kijamii ambao unaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi. Facebook imekuwezesha kujuana na watu wengi, kukutana na marafiki mliopotezana zamani na hata kujifunza mambo mengi. Hata makala hi unaweza kuwa umeipata kupitia facebok.

Pamoja na faida hizi, facebook imekuwa chanzo kikubwa cha watu wengi kupoteza muda kwani ina utegemezo mkubwa. Unaweza kujikuta kila siku unaangalia ni nini kinaendele kwenye facebook.

Kama utaacha kuangalia facebook kila mara, mambo haya matano yatatokea.

1. Utaacha kufa akili.

Kila mara unapotumia facebook ni kama akili yako inakuwa imekufa. Kwa sababu unajikuta akili yako yote imeingia kwenye mtandao huo na hivyo kushindwa kuona na kufikiria mambo mengine yanayoendelea. Kwa mfano unaweza kuwa umepanda gari safari nzima uko kwenye facebook tu na hivyo kushindwa kuona vitu vingine ambavyo vingekufanya ufikiri zaidi.

2. Utakamilisha kazi nyingi.

Kila mara unapoingia facebook hasa kwenye kuda wa kazi ni kama unajiibia muda wako wa kazi. Hivyo ukiweza kujidhibiti na ukapunguza muda unaoingia kwenye mtandao huu utakamilisha kazi nyingi.

3. Utawajua marafiki zako wa kweli ni kina nani.

Kupata marafiki kwenye mtandao ni rahisi sana. Unaweza kulike post zao au kuweka maoni kila mara na tayari mkawa karibu. Ila urafiki wa ukweli unahitaji zaidi ya hapo. Hivyo punguza muda unaotumia kwenye mtandao na ujue marafiki zako wa kweli ni watu gani.

4. Utaacha kujilinganisha na wengine na hivyo kujikubali.

Facebook inaweza kuwa sehemu ya kukufanya uone hakuna unachofanya cha maana. Hii inatokana na kuona wengine wakifanya mambo makubwa. Wakati mwingine unachokiona sio kweli.

SOMA; HIvi ndivyo mitandao ya kijamii inaharibu akili yako, kuwa makini.

5. Utagundua ulikuwa unatumika kibiashara.

Facebook zamani ilikuwa nzuri sana ila kwa sasa hivi wanatumia taarifa zako kuwauzia watu wa matangazo. Hivyo kila utakapoingia utakutana na matangazo na post nyingi za marafiki zako hutaziona tena. Kwa njia hii facebook wanakutumia wewe kibiashara.

Tumia mitandao ya jamii lakini usikubali mitandao hii ikutumie wewe.

Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.

Sehemu Tano Unazoweza Kupata Mtaji Wa Kuanzia Biashara.

Kisingizio kikubwa cha watu kushindwa kuanza biashara kimekuwa ni mtaji. Kila siku watu wanalalamika wanapenda kuanza biashara ila mtaji hawana. Lakini wakati huo hawafanyi jitihada zozote za kupata mtaji huo au kuanza kidogo na kufikia makubwa.

Kulalamika kwamba taasisi za fedha hazitoi mkopo kwa watu ambao hawana dhamana ni kupoteza muda wako. Nikuulize wewe akija mtu yeyote akakuambia nipe elfu kumi nitakurudishia nikiipata utampa? Ni vigumu sana. Kwa kuwa ni vigumu kupata mkopo kwenye taasisi za fedha leo JIONGEZE na sehemu hizi tano ambazo unaweza kupata mtaji wa kuanzia biashara.

1. Akiba zako mwenyewe.

Kama huna kazi ya kukupatia kipato tafuta hata kazi ya kibarua, ifanye na weka akibakatika kila unachopata, baada ya muda tumia akiba hii kuanza biashara.

2. Michango kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki.

Unaweza kukusanya mchango kutoka kwa ndugu jamaa na hata marafiki. Wape wazo lako na omba wakuchangie.

3. Kuanza na biashara ambayo haihitaji mtaji.

Kuna biashara nyingi ambazo unaweza kuanza bila ya mtaji. Anza na biashara hizi na ukishaanza kupata kipato kikubwa unaweza kuhamia kwenye biashara unayoitaka.

SOMA; Biashara tano unazoweza kuanza kufanya bila mtaji.

4. Kuandaa wazo zuri.

Kama una wazo zuri sana ambalo linaweza kufanyika ila huna mtaji, liandae wazo hilo vizuri sana na kisha angalia kampuni ambazo zinaweza kufaidika na wazo hilo kisha wauzie wazo hilo au wakupe sehemu ya faida itakayopatikana kwa wazo lako.

ANGALIZO; Sajili wazo lako kwenye mamlaka husika(BRELA) ili usije ukaibiwa wazo hilo.

5. Shiriki mashindano mbalimbali.

Kuna mashindano mengi sana yanafanyika siku hizi ambayo yanapambanisha mawazo bora ya kibiashara. Andaa wazo lako na ingia kwenye mashindano haya. Ukiweka wazo lako vizuri unaweza kuwa mshindi na ukapata mtaji.

Tumia njia hizo tano kupata mtaji wa kuanzia biashara. Kama unaona njia hizi hazifai au haziwezekani kwako endelea kukaa nyumbani na kuperuzi mitandao ya kijamii huku ukiendelea kupoteza muda.

Amua sasa kubadili maisha yako, chukua hatua.

NENO LA LEO; Kuhusu Kufikia MAFANIKIO MAKUBWA.

The greatest oak was once a little nut that held its ground!

 

Mti unaaonekana mkubwa siku moja ulikuwa mbegu ambayo ilishikilia ardhi.

Shilikia misingi yako na siku moja utafikia mafanikio makubwa. Usiyumbishwe wala kukata tamaa.

TUPO PAMOJA.

Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.

Kazi ndio msingi wa maendeleo. Na ili uweze kufikia mafanikio makubwa ni lazima ufanye kazi kwa bidii na maarifa. Sifa moja kubwa ya kufanikiwa kwenye kazi yoyote ni kupenda unachofanya. Kuna mambo mengi sana ambayo ukiyafanya kwenye kazi yako yanakuzuia kufikia mafanikio.

Leo JIONGEZE mambo haya matano ambayo ni marufuku kuyafanya eneo la kazi kama unataka kufikia mafanikio makubwa.

1. Kuonesha tabia ya hasira au kulipiza kisasi.

Mara kwa mara mtapishana kauli na mfanyakazi wako, mfanyakazi mwenzako au bosi wako. Kwa vyovyote vile tafuta njia ya kumaliza tofauti zenu kwa amani, ukiongea au kufanya mambo kwa hasira au kupanga kulipiza kisasi utaingia kwenye matatizo makubwa.

2. Majungu na kusengenya.

Maeneo mengi ya kazi hapa Tanza ia kuna majungu mengi sana. Usianzishe wala usishiriki kumpiga jungu mtu yeyote aliyepo kwenye eneo lako la kazi. Ni kumkosea heshima na hii itakufanya uingie kwenye matatizo.

3. Kudanganya.

Wafanyakazi wengi wamezoea kudanganya hapa na pale. Tatizo kubwa la kudanganya kwenye eneo lako la kazi ni kwamba itakubidi uishi uongo huo kwa muda mrefu kitu ambacho kitakuumiza.

4. Kuchukua sifa za wengine.

Kuna watu wanasubiri wengine wafanye kazi halafu wao ndio wanaokuwa wa kwanza kusema kama sio mimi hiki kisingewezekana. Usifanye hivi, utakosa ushirikiano kutoka kwa wengine. Kila mtu ana nafasi kubwa kwenye kukamilika kwa jambo lolote.

5. Usichome daraja.

Watu wengi wanaojiajiri wanatokea kwenye ajira. Zamani kidogo watu walikuwa wakiondoka kwenye ajira zao kwa ugomvi mkubwa na hivyo kuondoa kabisa ushirikiano. Wewe usifanye hivi, kama unakwenda kujiajiri hakikisha unakuwa na uhusiano mzuri na mwajiri wako kwani anaweza baadae kuwa mteja wako au akakuletea wateja. Mafanikio ya sasa yanatokana na ushirikiano mzuri uliojenga na watu.

Epuka kufanya mambi hayo matano kwenye kazi yako kama kweli unataka kupata mafanikio kupitia kazi hiyo.

Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.

Watu Watatu(3) Waliofukuzwa Kwenye Kampuni Walizoanzisha Wenyewe.

Unaweza kufikiri kuingia kwenye biashara na kujiajiri mwenyewe ndio njia nzuri ya wewe kuwa na uhuru kwa kile unachofanya. Inaweza isiwe kweli kwa sababu kwa jinsi hali ya biashara za kisasa ilivyo unaweza kujikuta kwenye hali ngumu sana.

Tena pale unapofikia kampuni ikawa kubwa na kuanza kuuza hisa, wenye hisa nyingi wanaweza kufanya maamuzi hata ya kukufukuza wewe japo wewe ndiye uliyeanzisha.

Hapa ni orodha ya watu watatu ambao walifukuzwa kwenye kampuni walizoanzisha wenyewe;

1. Steve Jobs, Apple

Steve Jobs alianzisha kampuni ya apple ila baadae alifukuzwa kwenye kampuni hiyo. Alikuja kurudishwa kwenye kampuni hiyo na kuleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia.

2. Ted Tunner, CNN

Ted Tunner alianzisha CNN, shirika la habari la marekani lakini baadae alikuja kufukuzwa kwenye shirika hilo.

3. Jack Dorsey, Twitter

Jack Dorsey ni mmoja wa waanzilishi wa mtandao wa kijamii unaoitwa twitter ila kwa sasa anaonekana hayupo tena kwenye mtandao huo kwani ameanzisha kampuni nyingine ya teknolojia.

Kuwa makini pale unapoanzisha kampuni yako yasije kukutokea mambo ambayo hukutarajia.

Nakutakia kila la kheri.

NENO LA LEO; Kuhusu Lifti Ya Kuelekea Kwenye Mafanikio.

There is no elevator to success. You have to take the stairs.

 

Hakuna lifti ya kuelekea kwenye mafanikio, ni lazima upande ngazi.

Watu wengi wamekuwa wakidanganywa sana kwamba kuna njia ya kupata mafanikio haraka, kama vile mtu anavyopanda lifti na kufika ghorofa ya kumi haraka.

Ukweli ni kwamba hakuna njia yoyote inayoweza kukuletea mafanikio haraka. Kama ilivyo kwamba itakuchukua muda kupanda ngazi mpaka ufike ghorofa ya kumi.

Usikate tamaa, SONGA MBELE.

Sababu 5 Kwa Nini Ni Marufuku Wewe Kukata Tamaa.

Katika maisha kuna wakati ambapo mambo huwa magumu sana. Ni katika nyakati hizi ambapo watu wengi hukata tamaa na kuacha kile ambacho walikuwa wanafanya.

Kwa kukata tamaa unashindwa kufikia mafanikio na pia unaona maisha yako kama hayana maana.

Leo JIONGEZE na sababu hizi tano kwa nini ni marufuku wewe kukata tamaa.

1. Bado hujafa.

Kama bado unaishi hii ina maana kwamba kila kitu kinawezekana. Hata iwe umeshindwa au kupoteza kiasi gani, jipange tena na utafikia mafanikio.

2. Kuna watu wengine walishafanya.

Katika jambo lolote ambalo linakushinda kufanya, kuna watu wengine walipitia changamoto kama zako ila waliweza kufikia mafanikio. Na kwa bahati nzuri sana watu hawa wameandika yote hayo kwenye vitabu, vitafute na uvisome.

3. Kuna watu wana hali mbaya kuliko wewe.

Wakati wewe unalalamika huna viatu kuna mwenzako hana miguu kabisa. Hivyo kukata tamaa na wakati kuna watu wana matatizo makubwa kuliko wewe na bado wanaishi utakuwa hujitendei haki.

USIKATE TAMAA2

4. Utawahamasisha wengine.

Kama ukiweza kufikia mafanikio licha ya changamoto unazokutana nazo utawahamasisha wengine nao kuweza kufikia mafanikio. Kama utakata tamaa na kuacha utawakatisha na wengine tamaa na kuwafanya wasijaribu kabisa.

5. Unastahili kuwa na furaha.

Kila mmoja wetu anastahili kuwa na furaha kwa sababu furaha hupewi na mtu bali inatoka ndani yako. Unapokata tamaa huwezi kuwa na furaha, badala yake utaona maisha yako kuwa kisirani. Ila kama utakomaa na kufanikiwa utakuwa na furaha idumuyo.

Sasa umeshajiongeza na sababu hizi tano za kutokata tamaa. Endelea kukomaa na utafikia mafanikio makubwa. Kama mambo yanazidi kuwa magumu badilisha mbinu ila sio kuacha kufanya kabisa.

Nakutakia kila la kheri.

Mambo 5 Muhimu Ya Kufanya Kabla Hujalala Leo.

Siku ya leo ndio inaelekea kuisha na kwa siku nzima ya leo umepitia mambo mengi sana. Kuna mengi umefanikiwa kufanya leo na pia kuna ambayo umepata changamoto kubwa.

Hata kama siku yako ilikuwa mbaya kiasi gani, kuna mambo mazuri uliyojifunza kwa siku hii.

Hapa kuna mambo matano muhimu unayotakiwa kufanya kabla ya kulala.

1. Fanya tathmini ya leo.

Fanya tathmini ujue umeitumiaje siku ya leo. Ni mambo gani umefanikiwa kufanya na ni yapi umeshindwa. Chukua kalamu na karatasi uandike mambo matatu uliyofanikiwa kufanya leo ambayo yamekusogeza kwenye mafanikio. Pia andika mambo matatu ambayo inabidi uyarekebishe.

2. Pangilia kesho yako.

Kabla ya kulala pangilia siku yako ya kesho. Andika mambo makubwa matatu unayohitaji kukamilisha kesho na uanze kuyafanyia kazi mapema kesho.

3. Pata muda wa kujisomea.

Tenga muda mchache wa kusoma kitabu, ndio kusoma kitabu cha kawaida.

4. Lala mapema.

Kwa kawaida watu wengi huchelewa kulala kwa sababu ambazo sio za msingi. Inaweza kuwa kuangalia tv au movie, kuperuzi mitandao mbalimbali na kadhalika. Ukilala mapema unaweza kuamka mapema ukiwa na nguvu.

5. Kaa mbali na mwanga wa vifaa.

Sasa hivi tunatumia vifaa vingi vinavyotoa mwanga mkali. Simu, kompyuta, tv hivi vinatoa mwanga mkali sana. Mwanga huu unakufanya uchelewe kupata usingizi. Hivyo ni vyema usitumie simu au kompyuta kitandani.

Anza kufanya mambo hayo matano leo na utaona mabadiliko kwenye maisha yako.

Tuko pamoja.

Faida 5 za matikiti maji kiafya

Tikiti maji  ni tunda ambalo linapatikana kwa wingi sana katika maeneo mbalimbali. Hili ni moja ya tunda ambalo linapatikana kila msimu wa mwaka.

TIKITI

Hata bei ya tikiti maji sio kubwa sana kiasi cha kwamba kila mtu anaweza kupata tunda hili.

Kuna faida nyingi sana za kula tikitimaji. Hapa utazijua faida tano za kiafya.

 

1. Inapunguza magonjwa ya moyo.

Matikiti maji yana kirutubisho ambacho huondoa sumu zinazosababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

2. Ni nzuri kwa mifupa yako.

Kirutubisho hiko kilichopo kwenye matikiti maji kinaweza pia kulinda mifupa na kupunguza magonjwa ya mifupa hasa kwa wazee.

3. Inapunguza mafuta mwilini.

Tafiti zinaonesha kwamba matikiti maji yana virutubisho ambavyo vinazuia mafuta kujikusanya mwilini.

4. Yanaongeza maji mwilini.

Unatakiwa kunywa maji mengi sana kwa siku. Ila ni wachache sana wanaoweza kunywa kiwango kikubwa cha maji. Ukila matikiti maji yanaongeza maji mengi mwilini.

5. Yanaimarisha kinga ya mwili.

Matikiti maji kama yalivyo matunda mengine yana vitamin c kwa wingi ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha kinga ya mwili.

Hizo ndio baadhi ya faida nyingi za matikiti maji. Ongeza idadi ya vipande unavyokula kila siku ili unufaike zaidi.

TUKO PAMOJA.

Biashara 5 Unazoweza Kuanza Kufanya Bila Ya Kuwa Na Mtaji.

Kikwazo kikubwa cha watu wengi kuingia kwenye biashara kimekuwa ni mtaji. Japo sio kweli kwamba mtaji pekee ndio kikwazo, lakini wengi wanaamini mtaji tu ndio unawazuia.

Lakini pia wakati huo ambao mtu hana mtaji hakuna juhudi kubwa anazofanya ili kuhakikisha anapata mtaji huo.

Sasa kufupisha habari leo JIONGEZE na biashara hizi tano unazoweza kuanza kuzifanya bila ya kuanza na mtaji wa fedha.

1. Biashara ya mtandao(Network marketing).

Hii ni biashara ambayo ni mkombozi kwa mtu yeyote ambaye ana kiu ya kufikia mafaniki. Hapa tanzania kuna makampuni mengi yanayofanya biashara hii kamA Forever living, Oriflame, GNLD, na mengineyo. Katika makampuni haya kuna ambayo unaweza kuanza na kiasi cha chini sana ambacho ni sawa na bure.

2. Biashara ya ushauri.

Je kuna kitu ambacho una utaalamu nacho? Je kuna kitu ambacho unapenda sana kukifuatilia na hivyo unakijua sana? Vizuri, kuna mtu anataka kukijua ila hajui aanzie wapi. Kwa wewe kutoa ujuzi na uzoefu wako unaweza kulipwa fedha.

3. Biashara ya taarifa(internet marketing).

Hii ni biashara ya kutoa taarifa kwa kupitia mtandao wa intanet. Unaweza kuwa na blog yako ambayo ni bure kuiendesha na baadae ukaanza kupata kipato kizuri kupitia mtandao.

Soma; jinsi ya kutengeneza fedha kwa kutumia mtandao wa intaneti.

4. Biashara ya uwakala wa mauzo(salesman.)

Kuna makampuni mbalimbali ambayo yanatumia mawakala kuuza bidhaa au huduma zao. Kwa wewe kujifunza na kuwa wakala wao unaweza kupata kipato kizuri kwa njia ya kamisheni.

5. Biashara ya udalali.

Hii ni biashara ambayo wewe unamsaidia mtu kupata kitu anachotaka na hana muda au uzoefu wa kukipata. Kama ukiweza kuifanya biashara hii kwa mbinu nzuri unaweza kutengeneza kipato kizuri.

Angalizo; Biashara hizi zinahitaji wewe ufanye kazi kwa bidii na maarifa na pia unaweza usione faida mapema. Ila ukiweka malengo na mipango mizuri utaona mafanikio makubwa baadae.

Uzuri ni kwamba unaweza kuanza biashara hizi ukiwa bado umeajiriwa au upo masomoni.

Nakutakia kila la kheri.

TUKO PAMOJA.

NENO LA LEO; Kuhusu Zawadi Kubwa Uliyopewa.

Everyone is gifted - but some people never open their package!

 

Kila mtu amezawadiwa, lakini baadhi ya watu hawafungui maboksi yao.

Kama unajiona wewe ni mtu ambaye huna bahati au huna kipaji chochote na kuna wengine ndio bora zaidi basi hujajijua vizuri. Kaa chini na utafakari kwa kina utaiona zawadi kubwa iliyoko ndani yako.

Nakutakia kila la kheri.

TUKO PAMOJA.

Mambo Matano(5) Ya Kufanya Siku Ya Jumatatu Ili Kuwa na Wiki Yenye Mafanikio.

Jumatatu ndio siku inayochukiwa na watu wengi kuliko siku nyingine yoyote ya wiki. Siku hii imepewa majina mabaya sana likiwemo BLUE MONDAY.

Jumatatu ni siku ambayo watu wanatoka kwenye mapumziko na kuanza tena kazi. Ni siku ambayo watu wanajua kuna siku tano za kazi mbele, na kama hupendi kazi yako ndio unazidi kupata msongo wa mawazo.

Leo JIONGEZE na mambo haya matano ambayo ukiyafanya siku ya jumatatu utakuwa na wiki yenye mafanikio makubwa.

1. Amka mapema na fanya mazoezi.

Kama mwishoni mwa wiki ulipumzika au kustareheka sana, jumatatu amka mapema na fanya mazoezi. Itakuwezesha kuianza wiki vizuri. Pia tumia muda huo wa asubuhi kupitia malengo na mipango yako ya wiki nzima.

Soma; faida 5 za kukimbia dakika 5 kila siku 

2. Pata kifungua kinywa.

Watu wengi sana hukosa muda wa kupata kifungua kinywa hivyo kuianza siku yao wakiwa wamechoka. Pata kifungua kinywa ili uianze wiki yako ukiwa na nguvu za kutosha.

3. Wahi kazini au kwenye biashara zako.

Tafiti zinaonesha jumatatu ndio siku ambayo watu wengi wanachelewa au kutokuhudhuria kabisa kazini au kwenye biashara zao. Sasa wewe usiwe mmoja wao, fika eneo lako la kazi mapema.

4. Jiandae kwa mambo usiyotegemea.

Kama umeajiriwa jumatatu unaweza kukutana na mabadiliko mengi sana kwenye eneo lako la kazi. Unaweza kukuta jukumu ulilokuwa unafanya unatakiwa uache na kukamilisha lingine lenye uhitaji wa haraka. Hata kama umejiajiri kutakuwa na mabadiliko ya hapa na pale tofauti na ulivyotegemea.

5. Kumbuka kuna jumanne.

Jumatatu inaweza kuwa siku ngumu sana kwako. Unajikuta na majukumu mengi na huku ukiwa haupo kwenye hali nzuri ya kufanya kazi. Usijiumize sana pale unaposhindwa kumaliza yote, kwa sababu sio mwisho wa dunia, kuna jumanne. Fanya kwa uwezo wako na endelea siku ya jumanne.

Naamini haya matano yataifanya jumatatu na wiki yako kuwa ya mafanikio.

Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.

HIZI NDIO HATUA KUMI ZA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KWENYE MAISHA YAKO



Angalia video hii fupi ambayo itakupatia hatua kumi za kuboresha na kubadilisha kabisa maisha yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.

NENO LA LEO; Kuhusu Ugumu Wa Kufanya Maamuzi.

It's not hard to make decisions when you know what your values are.

 

Sio vigumu kufanya maamuzi kama unaijua thamani yako au malengo yako.

Tunakosea katika kufanya maamuzi mengi kwa sababu tunayafanya bila ya kujua yataathiri vipi malengo yetu.

Nakutakia siku njema.

Mambo Matano Ambayo Watu Waliofanikiwa Hufanya Mwisho Wa Wiki.

Kwa taratibu nyingi za kazi kwa walioajiriwa na hata aliojiajiri mwisho wa wiki huwa ni siku za mapumziko. Kwa walioajiriwa wanaweza kuwa na siku mbili za mapumziko na waliojiajiri wanaweza kuwa na muda mfupi zaidi ya hapo.

Jinsi unavyoweza kutumia siku hizo za mwisho wa wiki inaweza kukufanya ufikie mafanikio au ushindwe kufikia mafanikio.

Hapa utaona mambo matano ambayo watu wenye mafanikio makubwa hufanya mwisho wa wiki.

1. Hupumzika.

Japokuwa siku hizi ni za mapumziko bado sio watu wote wanapumzika. Wengine hutumia muda huu kufanya kazi nyingine zaidi. Watu wenye mafanikio hupata muda wa kupumzika mwisho wa wiki.

2. Hufanya tathmini wa wiki inayoisha.

Watu wenye mafanikio hutenga muda mwisho wa wiki na kufanya tathmini ya wiki inayoisha. Huangalia ni kipi walishofanikiwa na ni wapi waliposhindwa.

3. Hupanga wiki inayoanza.

Watu wenye mafanikio hutumia mwisho wa wiki kuweka malengo na mipango ya wiki inayofuatia. Mipango hii huwawezesha kuwa na wiki yenye mafanikio makubwa.

4. Hujumuika na ndugu na jamaa.

Watu wengi wenye mafanikio huwa na kazi nyingi sana katikati ya wiki na hivyo kukosa nafasi ya kuonana na ndugu jamaa na marafiki. Hutumia mwisho wa wiki kujumuika na watu ambao hawajakuwa nao kwa muda mrefu.

5. Hukata mawasiliano.

Watu wenye mafanikio hutenga masaa machache mwisho wa wiki kukata mawasiliano yote. Hutumia muda huu kukaa na kutafakari maisha yao zaidi. Katika kukata mawasiliano huondoka kwenye mtandao, huzima simu na vifaa vingine vyote vya mawasiliano.

Na wewe unaweza kufanya mambo haya kila mwisho wa wiki na ukaboresha maisha yako zaidi.

Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.