NENO LA LEO; Kuhusu Kutabiri Kesho Yako.
The best way to predict your future is to create it!
Njia bora ya kutabiri kesho yako ni kuitengeneza leo.Usihangaike kupata utabiri kwamba maisha yako ya baadae yatakuwaje. Unao uwezo wa kuyatengeneza na kuwa kama vile unavyotaka wewe. Kujifunza zaidi tembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA.
Kila la kheri.
9/16/2014 01:00:00 PM | Labels: NENO LA LEO | 0 Comments
Sheria 10 Za Kuzingatia Kwenye Maisha.
Kuna sheria nyingi sana ambazo tunaishi nazo kwenye maisha yetu. Kuna ambazo tumezikuta kwenye jamii kwa asili na kuna ambazo zinatungwa na mamlaka husika.
Hapa kuna sheria kumi ambazo unatakiwa kuishi nazo kila siku ili kurahisisha maisha yako.
1. Ukifungua kitu, hakikisha unakifunga.
2. Ukiwasha kitu, hakikisha unakizima.
3. Ukivunja kitu, kubali umekivunja.
4. Kama huwezi kurekebisha ulichokivunja, mtafute anayeweza akirekebishe.
5. Ukikopa lipa.
6. Kama kuna kitu unakithamini, kijali.
7. Ukichafua, safisha.
8. Kama kitu sio chako, omba ruhusa kabla ya kukitumia.
9. Kama hujui jinsi ya kutumia kitu, jifunze kwanza au achana nacho.
10. Kama hakikuhusu usikiulizie maswali.
Kama unavyoona hizi ni sheria rahisi sana ambazo kama ukianza kuzifuata utaepukana na matatizo mengi sana. Anza kuzitumia sasa.
TUKO PAMOJA.
9/16/2014 12:00:00 PM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Mambo 10 Rahisi Unayoweza Kuanza Kufanya Leo Na Ukaboresha Maisha Yako.
Safari ya maisha ni safari yenye changamoto nyingi sana. Katika safari hii kuna milima na mabonde na hata visiki vinavyoweza kukukwamisha. Ili kuweza kushinda changamoto hizi kuna vitu vidogo vidogo sana unavyoweza kufanya kila siku na ukaboresha maisha yako.
Haya hapa ni mambo 10 unayoweza kuanza kufanya leo na ukaboresha maisha yako.
1. Kuwa na mtazamo chanya. Katika kila jambo linalotokea jua kuna kitu kizuri cha kujifunza au kunufaika.
2. Kunywa maji mengi. Sehemu kubwa ya mwili wako ni maji, ukosefu wa maji unaweza kukufanya upate matatizo ya kiafya.
3. Jenga tabia ya kujisomea. Tabia hii itakufanya uweze kufikiri zaidi na pia utajifunza zaidi. Kama huna kitabu cha kusoma bonyeza hapa na uweke email yako utatumiwa vitabu.
4. Jifunze kusema hapana. Matatizo mengi unayokutana nayo kwenye maisha yako yanatokana na wewe kukubali kila kitu unachokutana nacho au unachoambiwa. Anza leo kusema hapana.
5. Acha kutumia simu yako kwa muda. Simu za kisasa zimetufanya tuwe watumwa wa kila mara kuangalia nini kinaendelea. Anza leo kuzima simu yako japo kwa saa moja na utumie muda huu kufanya mambo mengine.
6. Pata kifungua kinywa. Watu wengi wanakosa kifungua kinywa kwa sababu ya haraka au kupunguza matumizi, usifanye hivi.
7. Usitumie zaidi ya unachopata, hakikisha matumizi yako yanakuwa pungufu ya kipato chako.
8. Acha kulalamika. Kama kuna kitu hukipendi kibadilishe, kama huwezi kukibadilisha achana nacho.
9. Omba msaada. Huwezi kufanya kila mwenyewe, unahitaji msaada wa watu wengi.
10. Kaa mbali na watu wenye kukatisha tamaa. Ukiwa karibu nao watakurudisha nyuma.
Maisha unayoishi ni yako na una uwezo wa kuyabadili na kuyafanya vile unavyotaka wewe. Anza leo kwa kufanya mambo hayo rahisi na utaona mabadiliko makubwa.
TUKO PAMOJA.
9/16/2014 07:29:00 AM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
Njia 10 Rahisi Za Kuondoa Msongo Wa Mawazo.
Msongo wa mawazo ni kitu kibaya sana kwa afya yako na hata kwa kazi au biashara yako. Unapokuwa na msongo wa mawazo huwezi kufanya maamuzi sahihi na hivyo kujikuta ukipata matatizo zaidi.
Japokuwa hakuna anayependa kuwa na msongo wa mawazo, maisha yetu ya kila siku yanatutengenezea msongo wa mawazo. Msongo huu unaweza kutokana na watu wanaotuzunguka au hata kazi tunazofanya.
Fanya mambo haya kumi ambayo ni rahisi sana na utaweza kuondoa msongo wa mawazo.
1. Pata muda wa kutosha wa kupumzika. Ukiweza kulala inakuwa bora zaidi.2. Fanya matembezi ya taratibu ukiwa mwenyewe kwa muda usiopungua nusu saa. Tembea sehemu ambayo unaweza kuona vitu vya asili kama majani au miti.
3. Chukua karatasi na uandike vitu kumi kwenye maisha yako ambayo unafurahi kuwa navyo, cha kwanza furahi kwamba bado unaishi.
4. Sikiliza mziki ambao unaupenda sana. Kila mtu ana aina yake ya mziki anaipenda.
5. Kaa kimya kwa dakika tano, usifikirie chochote kwa dakika hizo tano tu. Kuhakikisha hufikirii chochote hesabu pumzi zako.
6. Nyoosha misuli yako. Kama umekaa kwa muda mrefu nyanyuka na ufanye mazoezi kidogo yatakachangamsha misuli yako.
7. Fanya kazi ya kujitolea, tenga siku moja au muda wako na ufanye kazi za jamii za kujitolea. Kwa kutoa unajisikia vizuri zaidi.
8. Panga kukutana na marafiki zako uliopotezana nao muda mrefu. Kwa kukutana nao na kukumbushana mambo mliyokuwa mnafanya utajisikia vizuri.
9. Nenda sehemu ambayo hujawahi kwenda. Utaona mambo mapya na kujifunza mambo mapya yatakayokufanya uwe na mawazo mapya.
10. Angalia vichekesho, utacheka na kubadili hali yako ya msongo.
Fanya mambo haya kuondoa msongo wa mawazo. Sio lazima ufanye yote kwa wakati mmoja. Chagua machache unayoweza kuyafanya na yakabadili hali yako ya msongo wa mawazo.
Kila la kheri.
9/15/2014 07:27:00 PM | Labels: MBINU ZA MAISHA | 0 Comments
NENO LA LEO; Kuhusu Kufanya Mambo Mengi.
It's important to focus on one thing at a time. Even in the Roman times they understood this with their Proverb; "The man who chases two rabbits catches none."
Ni muhimu kufanya jambo moja kwa wakati. Hata wakati wa Roma walielewa hili kwa msoemo wao; mtu anayekimbiza sungura wawili, hushindwa kumsiha hata mmoja.
Chagua mambo machache na uyafanye kwa ufanisi mkubwa na utapata mafanikio makubwa sana.
TUKO PAMOJA.
9/15/2014 04:27:00 PM | Labels: NENO LA LEO | 0 Comments
Hili Ndilo Kosa Kubwa Tunalokwenda Kufanya Watanzania 2015.
Mwaka 2015 ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu sana na watanzania wengi umekaribia kabisa kufika. Huu ni mwaka ambao uchaguzi mkuu wa nchi yetu utakwenda kufanyika na hivyo wananchi kupata nafasi ya kuchagua diwani, mbunge na raisi ambaye tunaona anatufaa.
Mwaka 2015 umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kwa sababu wananchi wengi tumeaminishwa na kuamini kwamba baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 na chama tawala kuondoka madarakani maisha yetu yatakuwa mazuri sana. Ni imani nzuri sana ambayo tumekuwa nayo hasa ukizingatia hali ya nchi kiuchumi ipo chini sana ukilinganisha na rasilimali tulizonazo.
Pamoja na kuwa na imani hii nzuri, kuna kosa kubwa sana ambalo watanzania tutakwenda kulifanya mwaka huo 2015. Kosa hili litatugharimu tena miaka mingine mitano au hata zaidi ya hapo kama hatutaendelea kujifunza.
Kosa hili kubwa ni kutokuwa na vigezo vya kiongozi tunayemtaka sisi wananchi. Na kwa kukosa vigezo hivi tutarudia makosa ambayo tuliyafanya nyuma kwa kuchagua watu kutokana na umaarufu wao. Kutokana na kuangalia umaarufu tumechagua viongozi wengi ambao wameishia kutuangusha na kushindwa kutimiza ahadi zao wenyewe.
Ni lazima sisi kama wananchi bila hata ya kuambiwa na wanasiasa, tuwe na vigezo vya aina ya kiongozi tunayemtaka. Na hii ni kuanzia udiwani, ubunge na uraisi. Lazima sisi tuwe na vigezo vyetu kisha wale watakaojitokeza kuomba nafasi hizo tuwachuje kwa kutumia vigezo vyetu.
Ilivyo sasa ni kwamba wananchi hatuna vigezo vyetu, ila tunatumia vigezo vya wagombea watakavyotuletea na hivyo tunaweza kulinganisha baina ya mgombea na mgombea na kuamua kumchagua mmoja wao. Hapa ina maana kama wagombea wote ni wabovu tutamchagua ambaye ni ahueni. Na hapa ni kwa sehemu ndogo, shemu kubwa itatumia kigezo cha umaarufu.
Ni kigezo hiki cha umaarufu ambacho kinawafanya watu sasa hivi kuitisha mikutano ya waandishi kila kukicha kutangaza nia zao za kugombea uongozi. Ni kigezo hiki cha umaarufu ambacho kinawafanya watu kuzunguka huku na kule kutoa misaada ili waonekane wanajali sana.
Sasa watanzania tuache kufanya kosa hili ambalo litaendelea kugharimu maisha yetu.
Katika makala zijazo tutazungumzia ni vigezo gani tunaweza kuvitumia katika kila nafasi ya uongozi ili tuweze kupata viongozi bora.
Tanzania ni nchi yetu sote, unapopata ujumbe huu wajulishe na wenzako wote unaowafahamu ili tuweze kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu.
Usisahau kuweka email yako ili upate makala hizi moja kwa moja kwenye email yako.
TUKO PAMOJA.
9/14/2014 08:12:00 AM | Labels: SIASA, UONGOZI | 0 Comments
NENO LA LEO; Kuhusu Yasiyowezekana.
“Most things that we think are impossible in life, is because we have never tried them. So go for every dream and opportunity before making a judgement.”
“Mambo mengi tunayofikiri hayawezekani ni kwa sababu hakuna aliyewahi kujaribu kuyafanya, hivyo fanyia kazi kila ndoto yako kabla ya kujihukumu kwamba haiwezekani”
Nakutakia siku njema.
9/11/2014 01:34:00 PM | Labels: NENO LA LEO | 0 Comments
NENO LA LEO; Kuhusu upatikanaji wa FURSA
"Opportunities are found by those who look for them! The bee has a sting but honey too... so look at every negative and make a positive out of it."
"Fursa zinapatikana kwa wale wanaozitafuta, nyuki anauma ila ana asali pia.... hivyo angalia kwenye kila tatizo kuna njia ya kutokea"
Nakutakia siku njema.
9/09/2014 04:22:00 PM | Labels: NENO LA LEO | 0 Comments
NILICHOJIFUNZA LEO; Viongozi Mashuhuri Walioibadili Dunia.
Karibu kwenye kipengele hiki cha mambo niliyojifunza kwa siku husika. Kwa siku zinazokuja nitakuwa nakushirikisha yale ninayojifunza kuhusu uongozi kupitia kitabu WORLD FAMOUS LEADERS WHO RESHAPED THE WORLD.
Hiki ni kitabu kilichoeleza kwa kifupi baadhi ya viongozi ambao walifanya mambo makubwa duniani. Unaweza kujipatia kitabu hiki na ukaendelea kujifunza zaidi. Kava lake naweka kwenye picha hapo chini;
Viongozi hawa kuna waliofanya makubwa kwa wema kama Nelson Mandela na wengineo na kuna waliofanya makubwa kwa ubaya kama Adolf Hitler aliyesababisha vifo vya zaidi ya wayahudi milioni sita.
Kuna mengi ya kujifunza kupitia maisha na uongozi wa watu hawa.
Nakukaribisha katika safari hii ya kujifunza.
TUKO PAMOJA.
9/08/2014 04:10:00 PM | Labels: NILICHOJIFUNZA LEO | 0 Comments
NENO LA LEO; Kuhusu Hazina Ya Mwanadamu.
“More gold has been mined from the thoughts of men than has been taken from the earth. So dust off the cobwebs and use all those great ideas you have!”
“Dhahabu nyingi imechimbwa kwenye mawazo ya wanadamu kuliko iliyochimbwa ardhini. Hivyo futa futa utando uliokinga mawazo yako na anza kuyatumia mawazo yako kuleta mabadiliko.”
Nakutakia siku njema.
9/08/2014 03:55:00 PM | Labels: NENO LA LEO | 0 Comments
Je Vijana Wanaoingia Kwenye Siasa Wanaweza Kuwa Wakombozi Wetu?
Kumekuwa na wimbi kubwa la vijana hapa Tanzania ambao wanaingia kwenye siasa. Na kwanzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo baadhi ya vijana waliogombea ubunge walipata kuchaguliwa kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa vijana kuingia kwenye siasa.
Na hata kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 vijana wengi wameonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali. Na kwa kuwa mpaka sasa hatuna sheria inayoruhusu mgombea binafsi, vijana hawa wote ambao wana nia ya kugombea inawalazimu kupitia vyama vya siasa. Kwa sasa tuna vijana wengi sana ambao wameingia kwenye vyama mbalimbali vya siasa na wengine wamepata nafasi kubwa kwenye vyama hivi.
Swali kubwa la kujiuliza ni je vijana wengi kuingia kwenye siasa wanaweza kuwa wakombozi wa nchi yetu Tanzania? Natumia neno ukombozi kwa sababu naamini nchi yetu inahitaji ukombozi ili kutoka hapa ilipo. Inahitaji ukombozi kwa sababu tumefika hapa tulipo kutokana na uongozi mbovu na siasa na sera mbovu zilizowekwa na viongozi hawa wabovu. Na ukiangalia viongozi hao umri wao umekwenda sasa na hivyo vijana ndio watakwenda kuchukua nafasi zao siku za mbeleni.
Najiuliza swali hili kwa sababu tumeona baadhi ya vijana ambao wameingia kwenye siasa hizi wakiishia kutumiwa na baadhi ya watu na hivyo kujikuta wakishindwa kuleta mabadiliko yoyote. Tumeona baadhi ya vijana ambao walikuwa wakilalamikia uongozi mbovu ila wamepewa uongozi kwenye sehemu mbalimbali na kushindwa kuleta mabadiliko yoyote. Na vibaya zaidi wanaishia kuwa sehemu ya kitu walichokuwa wanakipinga.
Sina tatizo na kijana ambaye ameingia kwenye chama chochote cha siasa alichopenda yeye. Iwe ameingia CCM, CHADEMA, CUF au hata CHAUSTA. Kikubwa ambacho wananchi wanataka kuona ni mabadiliko ya kweli katika siasa zetu na hatimaye uongozi wa nchi yetu. Naamini mabadiliko haya yanawezekana kupitia vijana kama watajua ni kitu gani wanakwenda kufanya kwenye siasa hizi na kuepuka kutumika na wale ambao wapo kwenye mifumo hii kwa muda mrefu.
Wewe kama ni kijana ambaye umeingia kwenye siasa jiulize swali hili mara kwa mara na hakikisha unakuwa sehemu ya mabadiliko popote unapokuwepo.
Nakutakia kila la kheri katika harakati za kuleta mabadiliko katika taifa letu Tanzania.
TUKO PAMOJA.
Hakikisha hukosi makala mpya kila inapowekwa kwenye blog hii. Weka email yako hapo juu ili upate makala moja kwa moja kwenye email yako.
9/07/2014 11:11:00 AM | Labels: SIASA, UONGOZI | 0 Comments
NILICHOJIFUNZA LEO; Vita Kubwa Kuwahi Kutokea Afrika Ukiacha Vita Vya Pili Vya Dunia.
Ukiacha vita vya pili vya dunia vita kubwa ambayo imewahi kutokea Afrika ni vita ya pili ya Congo(Second Congo War)
Vita hii ilianza August 1998 na kutangazwa kumalizika July 2003 baada ya serikali ya mpito kushika madaraka.
Pamoja na kutangazwa kumalizika kwa vita hii bado mapigano na choko choko zinaendelea katika majimbo ya Kivu na Ituri.
Ni katika vita hii ambapo raisi wa Congo Laurent Kabila aliuawa na mtoto wake Joseph Kabila kushika madaraka ya kuongoza nchi.
Vita hii ilihusisha mataifa tisa ya Afrika na vikundi zaidi ya 20 vya wapiganaji.
Sababu ya vita hii.
Sababu kubwa iliyochangia vita hii ni mgogoro wa kimaslahi katika uchimbaji na biashara ya madini.Madhara ya vita hii.
Vita hii ndio vita kubwa zaidi kutokea barani Afrika ukiacha vita vya pili vya dunia. Mpaka kufika mwaka 2008 zaidi ya watu milioni 5.4 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na vita hii. Vifo vingi vilitokana na mauaji ya kuvita, huduma mbovu za afya na ukosefu wa chakula.Kuna mengi sana ya kujifunza katika vita hii. Kwa kifupi nimeweza kukuandalia haya kwa leo.
Tukutane tena wakati mwingine. Usisahau kuweka email yako ili upate makala hizi moja kwa moja.
Vyanzo;
WIKIPEDIA; Second Congo War.9/02/2014 05:43:00 PM | Labels: NILICHOJIFUNZA LEO | 0 Comments
Nilichojifunza Leo.
Nilichojifunza Leo ni kipengele kipya kitakachokuwa kinakujia mara kwa mara kupitia blog hii Makirita Amani. Ningependa kipengele hiki kiwe kinakujia kila siku ila siwezi kuahidi hilo kwa sasa.
Kupitia kipengele hiki utajifunza mambo mengi kuhusiana na UONGOZI, SIASA, UCHUMI, MAENDELEO na hata HISTORIA za nchi yetu Tanzania, bara letu Afrika na hata Dunia kwa ujumla.
Tutajifunza mambo mengi yatakayotusaidia kuelewa zaidi nchi yetu na dunia kwa ujumla wakati tunajiandaa kuwa viongozi bora wa nchi yetu.
Kupitia kipengele hiki mimi na wewe tutajifunza mambo yatakayotuandaa kuweza kuisaidia nchi yetu, wakati huo mimi naendelea kujiandaa kuwa raisi wa nchi yetu Tanzania.
Karibu sana katika blog hii maalumu kwa maswala ya uongozi na kuhakikisha hukosi machapisho yanayowekwa, weka email yako kwenye box hapo juu na utapokea makala moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa.
Naamini tutaendelea kuwa pamoja kwenye safari hii.
Nakutakia kila la kheri.
9/02/2014 09:00:00 AM | Labels: NILICHOJIFUNZA LEO | 0 Comments
Sababu Mbili Kwa Nini Tanzania Ni Nchi Masikini.
Kwa nini Tanzania ni nchi masikini? Pamoja na rasilimali nyingi tulizonazo, mlima mrefu, mbuga za wanyama, madini na hata ardhi kubwa kwa nini tunaendelea kuwa masikini?
Hili ni swali gumu sana maana hata raisi wa nchi mheshimiwa Jakaya Kikwete alikiri kwamba hajui kwa nini nchi yetu ni masikini. Sasa leo nataka tujadiliane nini kinatufanya tuendelee kuwa kati ya nchi masikini sana duniani licha ya rasilimali nyingi tulizonazo.
Katika moja ya vitabu vyake Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika kwamba ili tuendelee tunahitaji vitu vinne. Vitu hivyo ni WATU, ARDHI, SIASA SAFI na UONGOZI BORA. Katika vitu hivi vinne kuna viwili ambavyo tunavyo vya kutosha na viwili ambavyo tumekosa na ndio maana tunaendelea kuwa masikini.
Vitu viwili tulivyonavyo.
Katika vitu hivi vinne tunavyohitaji ili kuendelea, viwili tayari tunavyo, vitu hivyo ni;1. Ardhi. Tunayo ardhi kubwa sana ya kutosha. Sehemu kubwa ya ardhi ya tanazania bado haijatumika kabisa. Na sehemu kubwa ya ardhi yetu ina rutuba na hivyo inafaa kwa kilimo cha kila aina. Nenda katika kila mkoa utakuta kuna mazao fulani yanayokubali sana. Hata maeneo ya katikati ya nchi ambayo yana asili ya ukame bado kuna mazai yanakubali vizuri.
Lakini ardhi hii sasa iko hatarini kutoweka kutokana na ukosefu mwingine tutakaouona baadae.
2. Watu. Katika sensa ya mwaka 2012 tanzania ina watu zaidi ya milioni 45. Na wengi katika watu hawa ni vijana. Kwa watu wote hawa tulionao, kama wangeweza kutumiaka vizuri tungeweza kufikia maendeleo makubwa sana.
Vitu viwili ambavyo tumekosa.
1. Siasa safi. Kila nchi duniani inaendeshwa kwa siasa. Tanzania tuliwahi kuwa na siasa ya UJAMAA NA KUJITEGEMEA, ambayo ilikwenda vizuri sana mpaka pale ilipouliwa, tumewahi pia kuwa na SIASA NI KILIMO ambapo kilimo kilipewa kipaumbele kwa sababu ndio sehemu kubwa ya wananchi wanategemea kilimo. Lakini nayo haikudumu muda mrefu. Tuliwahi pia kuwa na SIASA YA UWEKEZAJI NA UBINAFSISHAJI ambapo tulishuhudia mashirika ya umma yakipewa watu binafsi na wengi wao kutoka nje ya nchi. Sasa hivi sina hakika tunaendeshwa na siasa gani.Tumekosa siasa safi na ndio maana tumeshindwa kutumia rasilimali zetu na hata watu wengi tulionao kuweza kufikia maendeleo kama taifa.
2. Uongozi bora. Hili ndio tatizo kubwa sana na ndio linazaa matatizo mengine yote. Tumekosa uongozi bora ambao unaweza kuwatengeneza na kuwatumia watu tulionao kuweza kufikia mafanikio. Tumekosa uongozi bora ambao utatengeneza siasa safi ambayo itatuwezesha kutumia watu wetu na rasilimali zetu vizuri.
Tunao watu wengi ambao wanashikilia nafasi za uongozi ila wamekosa sifa za uongozi. Watu hawa ndio wanafanya maamuzi mabovu na hivyo kutufanya tuendelee kuwa masikini.
Hii ndio sababu kubwa iliyonifanya niwe naandika kuhusu uongozi kwenye blog hii kila siku ya jumapili. Kama umekosa kusoma makala za uongozi zilizopita, bonyeza maandishi haya ili uweze kuzisoma.
Tufanye nini ili kuondoka kwenye umasikini huu?
Kwa kuwa tumeshajua mambo mawili muhimu tunayokosa ili kufikia maendeleo na kwa kuwa tumeshajua ukosefu wa uongozi bora ndio tatizo kubwa zaidi nashauri sisi wananchi tuchukue hatua ya kujua na kuchagua viongozi bora. Na nashauri hasa vijana tujifunze sana kuhusu uongozi na kisha tugombee nafasi mbalimbali za uongozi ili tuweze kuleta mabadiliko kwenye nchi yetu.Kukaa tu na kulalamika kila siku hakutakuwa na msaada kwetu binafsi na hata kwa vizazi vijavyo. Kuna chaguzi zinakuja mwaka huu na mwaka ujao, tutumie nafasi hii kujua ni viongozi wapi wanaotufaa na wapi wasiotufaa. Tukiendelea kufanya makosa haya katika uchaguzi wa viongozi tutaendelea kuwa masikini siku zote.
TANZANIA NI NCHI YETU SOTE, TUSHIRIKIANE KUIJENGA.
8/31/2014 10:20:00 AM | Labels: SIASA, UONGOZI | 0 Comments
Mambo Matano Ambayo Viongozi Bora Hufanya Kila Siku.
Karibu tena ndugu msomaji kwenye mtandao huu ambao umejikita kwenye kukujenga wewe kuwa kiongozi bora. Kwa siku za hivi karibuni hakujakuwa na makala mpya hapa kutokana na mambo yaliyoingiliana kidogo. Hata hivyo napenda nikukaribishe tena katika shule hii ya uongozi na kila jumapili utaendelea kupata makala za mambo ya uongozi.
Kama tulivyoona kwenye moja ya makala zilizopita kiongozi anatengenezwa na sio kuzaliwa. Ile dhana kwamba viongozi bora wanazaliwa sio kweli, bali viongozi bora hutengenezwa na mazingira waliyozaliwa na hata kukulia na pia elimu wanayoipata. Hivyo kama kuna mtu alikwambia wewe huwezi kuwa kiongozi kuanzia leo usikubali tena kauli hiyo.
Pia tuliona ni muhimu sana kila mtu kuwa kiongozi kwa sababu viongozi ndio wanaopata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote linalofanyika na binadamu. Iwe kazi, biashara na hata familia, unapokuwa na tabia za uongozi bora unapata mafanikio makubwa zaidi.
Leo tutaona mambo matano ambayo viongozi bora hufanya kila siku, anza kufanya mambo haya ili uweze kuwa na uongozi bora kwenye jambo lolote unalofanya.
1. Kujifunza.
Viongozi bora hujifunza kila siku na hii huwasaidia kujua mambo mengi na hivyo kuwasaidia katika kufanya maamuzi. Kama hujifunzi kila siku ni vigumu sana kuwa kiongozi bora. Viongozi bora hujifunza kwa kujisomea na pia hujifunza kutokana na uzoefu wao na uzoefu wa watu wengine.
2. Kupangilia siku yao.
Viongozi bora hupangilia siku yao kabla hawajaianza. Hujua watafanya kitu gani na katika muda gani. Kupangilia siku humwezesha kiongozi bora kukamilisha majukumu yake muhimu na kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda.
3. Kugawa majukumu kwa wengine.
Viongozi bora wanajua hawawezi kufanya kila kitu wao wenyewe, hivyo kila siku hutafuta njia za kugawa majukumu kwa watu wengine. Hii huwawezesha viongozi kubaki na majukumu machache ya msingi ambayo huyatekeleza kwa ufanisi mkubwa. Ili kuwa kiongozi bora acha kung'ang'ania kufanya kila kitu mwenyewe.
4. Kutengeneza viongozi wengine.
Viongozi bora hutambua kwamba kutengeneza viongozi wengine ni jukumu lao. Hivyo kila siku wanatengeneza viongozi wengine kwa kuwa washauri wazuri wa watu waliochini yao ili waweze kujiongoza na kuongoza wengine.
5. Huwasiliana vyema.
Viongozi bora hufanya mawasiliano mazuri kila siku kwa sababu wanajua mawasiliano yanaweza kuwajenga au kuwabomoa kama viongozi. Mawasiliano haya bora huyafanya wakati wanakutana na wengine, wakati wanaendesha vikao au mikutano na hata wakati wanafanya mawasiliano kwa simu. Viongozi bora hujua ni lugha ipi ya kutumia ili kuweza kufikisha ujumbe na ujumbe huo uwe na ushawishi mkubwa.
Mpaka sasa wewe ni kiongozi kwa sababu umeonesha nia ya kujifunza zaidi sasa unaelekea kwenye uongozi bora. Ongeza mambo hayo matano kwenye maisha yako ya kila siku na utaona mafanikio makubwa ya uongozi.
Kama una maoni yoyote tafadhali tushirikishe kwenye sanduku la maoni hapo chini.
Usisahau kuweka email yako kwenye box hapo juu ili kupata makala mpya kwenye email yako kila zinapochapishwa.
Nakutakia kila la kheri katika uongozi wako.
TUKO PAMOJA.
8/24/2014 09:25:00 AM | | 0 Comments

